Ijumaa, 17 Januari 2014

HIKI NDICHO ALICHOSEMA MAREHEMU CHACHA WANGWE



 Kimsingi mambo tunayotofautiana na Mhe. MBOWE ni haya yafuatayo:- MATUMIZI YA RUZUKU CHADEMA hupata ruzuku ya Tshs. 66,000,000 kwa mwezi (Milioni sitini na sita). Mimi nasema si haba hasa tukizingatia chama kilikotoka. Naamini kuwa kiasi hiki cha fedha kikisimamiwa vizuri kinaweza kukirahisishia chama kujieneza katika ngazi zote toka Tawi, Wilaya, Mkoa na Taifa. Si kweli kwamba matatizo yote yatamalizwa na fedha hizi lakini basi hata ofisi za chama zinaweza kuwa hai nchi nzima kitu ambacho kwa sasa hakipo. Mahesabu yanaonesha kuwa mtaji wa laki moja (Tshs.100,000/=) kwa wilaya moja nchini inatosha, hivyo kwa Wilaya 126 kwa mwezi jumla yake ni Tshs. milioni 12 (Tshs. 12,600,000/= ) zinahitajika ( Wilaya 126 x 100,000 kila wilaya = 12,000,000/=)Hata tukisema tupeleke kiasi hicho kwa kila jimbo la uchaguzi jumla yake ni Tshs. Milioni 23 (Tshs. 23,000,000/=) kwa maana ya majimbo 213 x 100,000 = 23,000,000/=. Mhe. MBOWE anasema hizo ni pesa nyingi sana kwa uimarishaji wa chama. Mimi nasema hapana, kiwango hiki kwa kila Wilaya au Jimbo la uchaguzi ni muafaka kwani haba na haba hujaza kibaba.Chini ya uongozi wa Mhe. MBOWE na wafuasi wake hawastaajabu kuwa kati ya Tshs. 374,144,000.40 zilizopatikana kama ruzuku katika ya Januari 1 na Juni, 30, 2008, Tshs. 350,000,000/= zilitumika Makao Makuu ya CHADEMA na Tshs. 25,000,000/= tu ndizo zilikwenda Wilayani kuimarisha chama.Mimi naona mgao huu unayatukuza Makao Makuu ya CHADEMA isivyostahili wakati huo huo ukidhalilisha chama nchi nzima. MADENI YA UCHAGUZI Kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Mhe. MBOWE alitufahamisha wanachama kuwa alikuwa anakidai chama US $ 181,949.00 sawa na Tshs. 218,338,546. Mpaka sasa chama kimekwisha mlipa Tshs. 175,000,000/=Baada ya kupata wadhifa wa Makamu Mwenyekiti, na kwa kuzingatia takwimu zionekanazo hapo juu katika kulinganisha matumizi ya fedha Wilayani na Makao Makuu niliamua kumshauri MBOWE asitishe kujilipa deni kutokana na fedha za ruzuku kwani siamini kuwa kulipa madeni yaliyopita kunaendana na utaratibu wa usimamizi wa fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa toka serikalini. Mhe. MBOWE alichachamaa na ndipo nilipomshauri kuwa kama ni hivyo basi atuthibishie pesa hizo anazodai alikikopesha chama ziliingia kwenye akaunti gani ya CHADEMA, kupitia hundi ipi, na lini? Nilimuomba pia kutaja ni kikao gani cha chama kiliidhinisha matumizi ya fedha hizo kwani kama hakuna ushahidi wa maidhinisho, ni dhahiri kuwa matumizi hayo hayakudhibitiwa na chama na kwa mantiki hiyo kuyafanya kuwa matumizi binafsi ya Mhe. MBOWE.Vilevile, nilimueleza kuwa matumizi ya fedha hizo alizodai alikikopesha chama yalikuwa yakinuka harufu ya UFISADI. Stakabadhi zote kuhusiana na matumizi hayo zilionesha kuwa gharama za aidha ununuzi na / au ukodishaji wa vifaa hivyo, hazikutofautiana na viwango wanavyolipishwa watalii kwa huduma kama hizo, kwa maana ya gharama ya juu sana.Na kwa kuwa hata baada ya kuwa Mhe. MBOWE amekwisha lipwa zaidi ya nusu ya deni alilodai kuikopehsa CHADEMA, vifaa vyote yakiwemo magari, vipaza sauti na kadhalika vimebakia kuwa mali yake binafsi, basi bila kumficha nilimueleza kuwa huko ni kukinyonya chama kwa kukigeuza kitega uchumi cha watu binafsi.Kuhusu suala la kulipa madeni kupitia ruzuku ya serikali, nilimuomba Mhe. MBOWE afuatilie kwa Msajili wa Vyama vya siasa ili tupate ufafanuzi kama kweli fedha za ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa, inaweza kutumika kulipia madeni ya viongozi wa vyama hivyo yatokanayo na uchaguzi ili CHADEMA isiathirike kisheria. Niseme kweli hapa kwamba, kwa vile wanaCHADEMA wengi walinichagua kuwa Makamu Mwenyekiti, na hata mimi mwenyewe tulikuwa wagombea wa nafasi za ubunge, udiwani n.k katika uchaguzi wa mwaka 2005 ningefarijika sana iwapo na sisi tungerejeshewa angalau chochote cha kufidia gharama zetu, kwa maana kwamba kama chama kimeamua kurudisha gharama hizo kiwalipe wote badala ya kulipa madeni kwa wateule wachache. UTEUZI WA WABUNGE WA VITI MAALUM Naamini ukweli wa suala hili hauna mjadala. Kwamba Mhe. MBOWE na wafuasi wake walighushi orodha ya majina ya viti Maalum badala ya kupeleka yaliyopendekezwa na Kamati Kuu sio siri. Naamini hata Mhe. MBOWE anakubaliana nami kuwa suala hili si moja ya siri anazodai nimevujisha! Yamesemwa mengi juu ya mtafaruku uliojitokeza kuhusu viti maalum hadi baadhi ya waasisi wa chama wakataka kujitoa na hivyo kumlazimisha Mwenyekiti Taifa ( FREEMN MBOWE) na Katibu Mkuu (DR WILBROAD SLAA) kukiomba radhi kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kwa kukiuka katiba, kanuni na maadili ya chama katika suala hili la kugushi viti maalum. Ni ukweli ulio wazi kuwa kitendo hicho cha upendeleo bado kina iumiza taswira ya CHADEMA. Chama kinaonekana kuendekeza ujanja ujanja kiasi kwamba watu na binti zao, wakwe zao, shemeji zao, waume wenzao, wachumba wa shemeji zao, wake wenza na kwa kiwango kikubwa watu wa kabila moja ndiyo wamekuwa sura ya CHADEMA bungeni.Katika hili nilichoweza kumueleza Mhe. MBOWE ni kuwa chaguzi mbalimbali tangu za Mitaa, Ubunge na Urais zinakaribia ni vizuri tufanye bidii kusambaza nguvu zetu nchi nzima tuwe na mtaji wa kura maeneo mengi ili kashfa kama hii isijirudie. Hii ni kwa msingi kuwa chama kikijitanua kutakuwa hakuna sababu ya kuwaona watu wa eneo fulani tu kuwa ndiyo mhimili wa CHADEMA na hivyo zikitokea fursa itakuwa rahisi chama kuwakilishwa na mtandao wake mpana badala ya koo au kabila fulani.Sasa kwa kuwa kuimarisha chama kitaifa maana yake ni matumizi ya fedha, nalo hili likawa nongwa ingawa kwa mtazamo wa Makao Makuu kulipa madeni kwa wateule wachache si nongwa. Cha ajabu ni kwamba Mhe. MBOWE hakukana kuwa hili la viti maalum na hata upangaji wa ajira kwa ukabila una leta athari mbaya kwa mustakabali wa CHADEMA Katika maongezi yangu nae nilikuwa wazi nilipotahadharisha kuwa: 1. Watanzania wakiendelea kuona kwamba CHADEMA inaendeshwa kwa misingi ya kikabila hawatajiunga na chama chetu na tutakosa wafuasi. 2. Watanzania wakiona kuwa sisi tumeweka mbele ukabila kuliko utaifa hawatatupa madaraka na kutawala kwa kuhofia yale yanayotokea nchi jirani kama Rwanda, Burundi, Kenya na kadhalika ambako nafasi za raia wote zimehodhiwa na kabila moja na hatma yake watu wamechinjana kama kuku kwa kupinga hilo. Pia nilimwambia kwamba, kwa jinsi sura ya uteuzi wa Wakurugenzi na watendaji wengine wa Makao Makuu inavyoonekana, sasa tayari chama chetu kimebatizwa jina la CHAMA CHA WACHAGA, na hii si kuwatendea haki raia wengine na makabila yao ambao wataonekana kama punguani kujihusisha na chama na ukabila.Yote haya ninayosema kuhusu ukabila, upendeleo na kadhalika sio dhana tu. Kufuatia malalamiko mengi yaliyokuwa yakisikika nchi nzima kuhusu masuala haya, Kamati Kuu ya CHADEMA ilikwisha unda Tume kutafuta ukweli wa mambo hayo. Tume hiyo ya watu watano iliongozwa na Mhe. Merky Lugendo Mziray ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA nayo imekwisha toa taarifa yake kwamba Makao Makuu ya CHADEMA yanatawaliwa na ubaguzi wa kikabila, kidini na kielimu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD

KARIBU KWENYE BLOG YETU YA KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD