Jumanne, 14 Januari 2014

TUNDU LISSU AKIWA NDANI YA GPL: ZITTO ATATIMULIWA, BUNGE LA SAMWELI SITA LILIKUWA LA KISASA


Zitto atatimuliwa
MNADHIMU Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tindu Lissu, amesema Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe atakoma kuwa mwanachama mara tu baada ya mahakama itakapolirudisha suala hilo chamani.
Katika mahojiano maalum ndani ya chumba cha habari cha Global Publishers mchana huu, Lissu ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, anasema ni vigumu kwa Zitto kuendelea kuwa mwanachama kutokana na mambo aliyoyafanya.




...Akiongea mbele ya timu nzima ya wahabari wa Global.
...Wakiendelea kumsikiliza kwa makini.
Baadhi ya wafanyakazi wa Global Publishers Ltd wakimsikiliza Tundu Lissu.
...Akifafanua jambo.
...Akiongea na Mkurugnezi wa Global Publishers, Eric Shigongo, kabla ya kuagana naye.
...Akiagana na Mkurugenzi wa Global.
...Akiangalia kadi ya mwanachama wa Chadema, Walusanga Ndaki (kushoto) ambayo amekuwa nayo tangu mwaka 1992.

“Zitto alikuwa anataka uenyekiti wa chama chetu, siyo jambo baya, lakini alishiriki kutengeneza waraka wa siri, siri kubwa, ambao haukubaliki. Alimtuhumu mwenyekiti wetu kuwa hana elimu, malaya, mnunuzi mkuu wa mali za chama, fisadi na mambo mengine mengi ya namna hiyo. Huu ni uongo mkubwa, hatuwezi kuukubali.
“Ni vigumu kuzungumzia umalaya wa mwenyekiti wetu lakini nadhani hayo ni mambo ya chumbani ambayo kwa vyovyote huwezi kuyaunganisha na uongozi. Hayo ni mambo binafsi, kama tungekuwa tunalinganisha mambo hayo, sijui tungesema nini kuhusu Rais Nelson Mandela na Bill Clinton wa Marekani ambaye alikumbwa na kashfa katika mojawapo ya vibaraza vya Ikulu ya White House,” alisema.
Lissu, alisema Zitto, akiwa Naibu Katibu Mkuu, anafahamu kuwa kila jambo linajadiliwa na Kamati Kuu ambayo yeye ni mjumbe na kwamba tuhuma zote dhidi ya Mwenyekiti na Katibu Mkuu ni uongo.
Kuhusu ukomo wa nafasi ya Uenyekiti wa Chadema Taifa, alisema waraka wa mabadiliko ya katiba ulitolewa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu mwaka 2006, Shaibu Akwilombe aliousambaza kwa wenyeviti wa Wilaya na Mikoa Tanzania nzima uliowataka kuridhia kuondoa kipengele cha ukomo wa nafasi hizo, vinginevyo chama hicho kingekufa kwa vile kusingekuwa na kiongozi halali hadi wakati huo.
“Chama chetu kilitaka kuondoa ukomo huo kwa sababu awali, kilisema kila baada ya miaka kumi viongozi wangetoka, lakini baada ya kulitazama kwa makini, tukagundua kwamba tungekuwa hatuna viongozi kama tungeendelea na utaratibu ule kwa sababu ingefikia baada ya miaka kumi, viongozi wote wanatoka, sijaona chama hicho kama kipo hapa nchini,” alisema Lissu.
Yeye ni msumbufu bungeni?
Kuhusu kuonekana kama yeye ni mtu wa vurugu bungeni, Lissu alisema siyo kweli, bali ni mtu mwenye kusimamia kanuni na ndiyo maana anaonekana kuwa hivyo.
Alisema kilichopo hivi sasa ni kuwa ndani ya Bunge la Kumi kuna wabunge wengi wajuaji wameingia (sio wajuaji kama tunavyosema uswahilini, ni wajuaji kwa maana ya wajuaji hasa wa mambo).
Alisema wanajua kutafsiri kanuni na wanazisimamia. “Nadhani ni bunge hili ndilo wananchi wamejua baadhi ya lugha za bunge kama Mwongozo wa Spika na kadhalika, wananiona nina vurugu kwa sababu ninasimamia ukweli.
“Katika Rasimu hii ya Katiba, kumefanyika mabadiliko mara tatu, wanaongea wanakubaliana, lakini baadaye mimi ninasimama na kusema tatizo. Na nikuambie, hoja zote zilizosababisha kufanyiwa kwa marekebisho katika mara zote tatu, zilianza kwenye mkoba wangu, kwenye kalamu yangu, maoni yote kuhusu katiba niliyaanzisha mimi na kuyafanya kuwa ya kambi rasmi ya upinzani bungeni,” alisema Lissu.
Alisema Rais Jakaya Kikwete amekuwa akimshambulia kwa kumuita kama mwanasheria msumbufu, lakini kwake ni fahari kwa sababu wakati anamsema hivyo, pia mapendekezo yake yamekuwa yakifanyiwa kazi kila mara.

Samuel Sitta na Anne Makinda nani zaidi?
Akizungumzia kuhusu bunge lililokuwa chini ya Spika Samuel Sitta na wa sasa, Anne Makinda, Lissu alisema enzi za Sitta bunge kama taasisi, lilikuwa na nguvu na lenye hadhi, lakini hili la sasa, spika amekuwa akilitumia kwa ajili ya kuitetea na kuilinda serikali badala ya kuisimamia na kuiwajibisha.
Alisema endapo bunge lililo chini ya Mama Anne Makinda lingekuwa linaendeshwa kwa manufaa ya wananchi, mambo mengi makubwa yangetokea, kwani kuna madudu mengi sana yaliyofanyika kuliko hata kipindi cha Sitta.
“Chukulia Operesheni Tokomeza Ujangili kwa mfano. Kama mambo yengekwenda sawa, serikali nzima ingewajibika, tofauti na sasa tunapoambiwa mawaziri wanne tu wamejiuzulu.
“Ile ilikuwa ni operesheni ya kijeshi, ni kama jeshi lilikuwa vitani. Ni nani anatangaza vita? Ni Rais, lakini pia rais kabla ya kuliingiza jeshi vitani, ni lazima tamko hilo lije bungeni lijadiliwe, hatujaletewa bungeni kulijadili, lakini jeshi limeingia vitani dhidi ya raia, wameuawa Watanzania wengi sana, wengi wamejeruhiwa, wengine kupata vilema vya maisha.
“Kama ripoti ya kamati ya Lembeli ingejadiliwa kwa uwazi, serikali nzima ingewajibika. Hii yote ilitokana na utendaji usioridhisha wa spika wetu wa sasa, Anna Makinda,” alisema.

SOURCE GPL

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD

KARIBU KWENYE BLOG YETU YA KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD