*Wasema kisipochukua hatua kitafika 2015 kikiwa dhaifu
SAFARI ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuelekea katika
uchaguzi mkuu wa 2015 imeelezwa kuwa ni yenye kutia shaka na
kimetabiriwa kufika mwaka huo kikiwa dhaifu.
Mwenendo wa matukio ambayo umma umeendelea kuyashuhudia ndani chama
hicho wiki hii, msingi wake ukiwa ni kuvuliwa uongozi Zitto Kabwe na
kuvuliwa uanachama kwa Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba, ndiyo
yaliyoibua hisia za namna hiyo miongoni mwa umma na jamii ya wasomi
walioko ndani na nje ya chama hicho.
Tayari baadhi ya wasomi na wanasiasa wenye ushawishi hapa nchini,
wakiwemo viongozi wa kada mbalimbali, wamekwisha kukaririwa kwa nyakati
tofauti wakieleza kuona hatari ya kifo inayokikabili Chadema, kutokana
na uamuzi wake huo wa kuwavua uanachama makada wake wawili na kutishia
kuchukua uamuzi kama huo kwa Zitto.
Ndani ya Chadema na katika Kamati Kuu ya chama hicho, baadhi ya wajumbe
wake nao wamekaririwa kutoa kauli zinazoonyesha kuona hatari ya kifo
inayokikabili chama chao.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchugaji Peter Msigwa, amekaririwa ndani ya
Kamati Kuu ya chama hicho hivi karibuni, akisema kuwa ni heri chama
hicho kipoteze Uchaguzi Mkuu wa 2015, lakini Zitto aondolewe.
Mbali na Msingwa, miongoni mwa wasomi wanaoheshimika hapa nchini, na
makada wa chama hicho, Mabere Marando na Profesa Mwesiga Baregu, nao
wametoa kauli za kukionya chama hicho juu ya uamuzi wake huo na kueleza
hatari wanayoiona mbele.
Marando amesikika ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho akisema kuwa, anaona mwelekeo ule ule wa NCCR-Mageuzi kuipata Chadema.
Ni kutokana na hilo, matukio ya hivi karibuni kabisa ya kutekwa na
kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Temeke, Joseph Yona,
lakini pia kuzuka vurugu ndani ya Kamati Kuu na lile la wafuasi wa
chama hicho walio katika pande mbili zinazopingana, kupigana nje ya
Mahakama Kuu ya Dar es Salaam, ambako Zitto alikuwa akitafuta haki yake
ya uanachama, yanafananishwa na yale yaliyopata kutokea ndani ya chama
cha NCCR-Mageuzi kati ya miaka ya 1990 na 2000.
Inaelezwa kuwa miongoni mwa mambo ambayo yalichangia chama cha
NCCR-Mageuzi, ambacho kilikuwa chama kikuu cha upinzani nchini kupoteza
nguvu zake wakati huo, ni migogoro ya kiuongozi ambayo ilisababisha
watu kutwangana hadharani, kama ilivyo sasa kwa Chadema.
Tayari Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi,
amekitaka Chadema kujiepusha na vurugu na uvunjifu wa amani wakati
kinapotatua mgogoro wake na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto
Kabwe.
Wakati hayo yakitokea, huko Kigoma baadhi ya wananchi nao wamekaririwa
wakieleza kufedheheshwa na kauli iliyotolewa na baadhi ya viongozi wa
Chadema ya kumuita Mbunge wao kuwa ni Mbunge wa Mahakama na wametamka
bayana kwamba iwapo Zitto atatimuliwa, chama hicho kisahau kuungwa
mkono mkoani humo.
Askofu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana anayetoka Mkoa wa Kigoma, Dk.
Gerald Mpango, ambaye amekuwa mpenzi mkubwa wa siasa za mageuzi na
ameshiriki mikakati mingi ya kuijenga Chadema, amesikika akisema kuwa
hatua ya kumtoa Zitto haitakiacha salama chama hicho, licha ya kuwahi
kufanya hivyo kwa Dk. Amani Kabourou na David Kafulila.
Wasomi ambao wameelezea matukio yanayotokea ndani ya Chadema,
wameonyesha shaka kama chama hicho kitaweza kufanya vizuri katika
uchaguzi mkuu ujao na kuonya kuwa kisipotafuta suluhu mapema, kuna
dalili za kuanguka.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prosper Ngowi, aliliambia Gazeti
hili kwamba nyakati hizi si sahihi kwa chama hicho kuweka kipaumbele
migogoro.
“Katika hili naweza kusema kuwa hiki si kipindi kizuri kwa Chadema
kulumbana, kwasababu kama tunavyofahamu kuwa tunaelekea katika kipindi
cha uchaguzi mkuu mwaka 2015, nilitarajia Chadema kama chama kikubwa
cha upinzani kingetumia muda huu kujiimarisha zaidi kiweze kufanya
vizuri katika uchaguzi wa 2015.
“Priority (kipaumbele) yao kwa sasa kilitakiwa kiwe kuangalia namna
nzuri ya kuweka mikakati imara ya kuongeza madiwani, kuchukua viti
vingi zaidi katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika
mwaka huu, lakini pia kushinda majimbo mengi zaidi na ikiwezekana hata
katika nafasi ya urais,” alisema Profesa Ngowi.
Alisema anashangazwa na kitendo cha sasa cha kuweka malumbano kama
kipaumbele chao, hali ambayo inawadhoofisha katika kupanga mikakati
imara ya ushindi.
“Wataalamu wa masuala vya vyama vingi wanasema kuwa kila lengo kubwa la
chama cha upinzani, ni lazima katika kutafuta hiyo dola kuwe na
mipango ya muda mrefu, sasa naona kama Chadema, moja ya chama kikubwa
cha upinzani wameacha kufanya hilo kwa sasa na wameweka nguvu kubwa
katika kutafuta migogoro, jambo ambalo linaweza kuwaangusha,” alisema
Profesa Ngowi.
Alisema mgogoro uliopo kwa sasa hawezi kusema mshindi ni nani, bali
busara inapaswa kutumika kumaliza tatizo lililopo kuweza kupata
mwelekeo mzuri kuelekea mwaka 2015.
“Naweza kusema kuwa bado wana nafasi ya kusuluhisha hadi kufikia
uchaguzi wa serikali za mitaa na kuelekea uchaguzi mkuu ujao,” alisema
Profesa Ngowi.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Peter
Maina, alisema mambo yaliyojitokeza yataifikisha Chadema 2015 ikiwa
dhaifu.
Alisema mgogoro uliojitokeza mpaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
kukimbilia Mahakamani, umetokana na uongozi wa chama hicho kushindwa
kutumia busara kutatua mgogoro huo mapema.
“Niseme tu kwamba kuna watu ndio wameufikisha huu mgogoro hapo ulipo,
ilikuwa rahisi kutumia busara kuumaliza pale wenzake na Zitto (Dk.
Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba) walipokiri kuandaa waraka na kusema
ulikuwa siyo kwa nia mbaya.
“Lakini kuna watu wazito ndani ya Chadema kama kina Profesa Safari,
Mabere Marando na wengine walipoona jambo hili inasemekana waliomba
suluhu ya haraka, lakini inaonekana kuna watu upande wa chama hicho
hicho hawataki suluhu na matokeo yake ndiyo haya ya kupelekana
Mahakamani,” alisema Profesa Maina.
Alisema kitendo cha kulumbana nyakati hizi ni kusababisha chama hicho kuingia katika uchaguzi mkuu kikiwa dhaifu.
“Huu ni wakati wao wa kutafuta suluhu, naamini chama hakitakufa, lakini
kitafika katika uchaguzi mkuu kikiwa dhaifu, hakitakuwa na nguvu kama
ya awali, lazima viongozi wa Chadema wafahamu kuwa wakati mwingine
haraka haina faida, uharaka uliotumika kushughulikia mgogoro haukuwa na
faida.
“Kwa mfano, angalia Katibu Mkuu wa chama, Dk. Willibrod Slaa
alivyofanya kipindi kile, badala ya kusuluhisha mgogoro, yeye anakwenda
jimboni kwa Zitto kufanya mkutano, hapa inaonekana dhahiri hakuwa na
nia ya kuleta suluhu, bali kuendeleza mgogoro, nafikiri busara
hazikutumika toka awali na ndiyo maana leo hii mgogoro umekuwa mkubwa,”
alisema Profesa Maina.
Katika hatua nyingine, Profesa Maina alisema kauli ya mwasisi wa chama
hicho, Edwin Mtei, ya kusema Zitto hatakiwa ndani ya Chadema,
inakiumiza zaidi chama, kwani haionyeshi demokrasi katika chama.
“Kauli ya Mtei inazidi kuonyesha nia ovu waliyonao baadhi ya watu ndani
ya Chadema, kusema Zitto akatafute chama siyo maneno ya kuonyesha
ukomavu kidemokrasia, niseme kwamba Mtei yeye anakiumiza zaidi chama,
huu siyo wakati wa kulumbana ni wakati wa kutafuta suluhu kurudisha
heshima ya chama.
Akizungumzia kitendo cha Zitto Kabwe kukimbilia Mahakamani alisema
mbunge huyo amefanya hivyo kujikinga kutokana na hatua zilizopangwa
kuchukuliwa dhidi yake.
“Kitendo cha Zitto kukimbilia mahakamani si kitendo cha ajabu bali
amekwenda sehemu aliyoona haki itatendeka dhidi yake, unapoona mambo
yanafanywa na mpinzani wako na unaona unaweza usitendewe haki una haki
ya kwenda Makahamani kwahiyo wanaosema kwamba Zitto amekosea si kweli
kwasababu yeye si mtu wa kwanza kwenda Mahakamani,” alisema Profesa
Maina.
SOURCE: Mtanzania
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni