Ijumaa, 12 Januari 2018

SUGECO IMEFUNGUA NJIA KWA VIJANA WAJASIRIAMALI KATIKA SEKTA YA KILIMO BIASHARA

Vijana wengi wa Tanzania tuna shida kubwa katika bongo zetu. Tumegeuka kuwa jamii ya kulaumu na kulalamika badala ya kuchukua hatua.Tunapenda urahisi. Tunasahau kuwa zama zimebadilika. Hatufikirishi vichwa vyetu kujaribu kutumia japo sehemu ndogo ya elimu tuliyoipata chuoni kutafuta fursa za kukamata.

Badala yake tumekaa tukibweteka tukiamini siku moja tutapata kazi ya ndoto zetu huku siku zikizidi kuyoyoma bila mafanikio. Tumekuwa mizigo kwa wazazi wetu badala ya kuwa msaada. Hakuna mawazo mapya tunayotoa. Zaidi tunatamani utanashati bila kuwa na pesa mfukoni. Kazi za kuchafuka hatuzitaki tena hata kama zinatengeneza pesa kiasi gani. Usomi wetu  umetufanya tuchague kazi.

Kijana asiyeenda shule,  unakuta ana uwezo mkubwa zaidi wa kutengeneza pesa,  kuliko msomi aliyehitimu chuo kikuu. Kijana asiyefika chuo kikuu hachagui kazi na vilevile yuko tayari kumtumia msomi kuuliza kitu asichokijua, lakini msomi yeye kwa upande wake hayuko tayari kujifunza kutoka kwa kijana asiyebahatika kufika chuo kikuu.

Tuna tatizo kubwa sana. Vijana wengi tumekosa mawazo mapya ya Ujasiriamali.  Bongo zetu zimelala. Hatuoni fursa mpya pamoja na kwamba fursa hizo zimejaa tele mtaani. Tunahitaji kufunguliwa vichwa vyetu na macho ili tuweza kuondolewa tongotongo zinazotufanya tushishindwe kuona fursa.

Changamoto ya kushindwa kuona fursa  haiwakabili tu vijana wasomi waliyohitimu vyuo mbalimbali pekee yao bali hata wazee wetu waliyostaafu kutoka kwenye utumishi wa umma au sekta binafsi nao wanakabiliwa na tatizo hili.

Utastaajabu kumwona mstaafu namna anavyohangaika mtaani kuyakabili maisha yake mapya. Hawezi kufanya kazi nyingine zilizo nje ya fani yake. Matokeo yake baada ya kustaafu utumishi wake,  anakuwa hana uwezo tena wa kuratibu na kusimamia mradi utakaompatia pesa na kumwezesha kuishi maisha yanayofanana na yale aliyokuwa akiyaishi alipokuwa kazini.

Mstaafu anaishi maisha ya ajabu kabisa pamoja na kwamba,  alipatiwa mafao yake yote na mfuko wake wa hifadhi ya jamii. Amekosa elimu ya ujasiriamali. Pesa za mafao yake ya kustastaafu,  anaingiza kwenye miradi mfu. Matokeo yake anapata anguko kubwa lisilo kuwa na mfano.

Lakini yote hii ni kwa sababu kulikuwa hakuna taasisi au watu waliyojitoa sawasawa kunoa bongo za watu wengine ili wawe na uwezo kujitegemea mara baada ya kustaafu au kumaliza viwango mbalimbali vya elimu.

Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO),  kwa upande wao waliliona hili na kuamua kwadhati kabisa kujitoa kuwasaidia wahitimu wa vyuo mbalimbali na vijana wasiyowahitimu ili waweze kujiajiri wao wenyewe katika sekta ya Kilimo Biashara.

Kupitia SUGECO, vijana wamekuwa wakifundishwa stadi mbalimbali za kilimo biashara ikiwemo mbinu bora za kuendesha kilimo cha kisasa, kilimo chenye tija, ufugaji bora,  Uongezaji wa thamani wa mazao ya Kilimo na mifugo, Usindikaji wa bidhaa mbalimbali za kilimo, uendeshaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuondoa tongotongo katika bongo za vijana, kuwawezesha vijana wahitimu wa vyuo kuwa na miradi yao binafsi na kupata fursa ya kusimamiwa kwa ukaribu na hatua kwa hatua hadi mradi utakaposimama.

Si hivyo tu bali pia SUGECO wanajishughulisha na utoaji wa ufadhili wa mashamba Kitalu au Greenhouse kama ilivyozoeleka  na wengi  kwa vijana ili kuwawezesha  kuendesha shughuli za kilimo chenye udhibiti wa magonjwa. Kana kwamba haitoshi,   SUGECO wanaendesha programu kabambe ya kuwapeleka vijana nchini Israel kushiriki mafunzo kwa vitendo katika sekta ya Kilimo. Kila mwaka kuna kundi la vijana wasiyopungua 30 wanapelekwa Israel.

Ukikaa na vijana waliyopata fursa ya kwenda nchini Israel na ukasikiliza shuhuda zao, utabaini wazi kuwa sisi watanzaia bado hatufanyi kazi kabisa. Tunapoteza  muda wetu mwingi  kizembezembe.  Wenzetu kule wanachunga sana muda wao na kujali zaidi kazi. Kwao siku zote muda huwa huwatoshi kutekeleza majukumu yao,  hivyo wanajitahidi kuitumia kila dakika inayopatikana kufanya kitu kinachoonekana. Muda kwao una thamani kubwa sana hivyo haupaswi kuchezewa hata kidogo.

Siku zote waisrael  wanaamini kuwa hakuna mtu atakayekufa kwa kufanya kazi. Kwa hiyo ukiwa Israel masaa mengi utayatumia kwa ajili ya kufanya kazi. Siku ya mapumziko kwao ni siku moja tu katika wiki na ni siku ya jumamosi ambayo pia siku hiyo wanaitumia kwa ajili ya kukufanya Ibada.

Kuwa meneja Israel ni tofauti sana na kuwa meneja katika nchi zetu za afrika ambapo meneja anakuwa anaongoza kwa  kula bata,  kule ukiwa meneja hakuna kula bata, bali  meneja unakuwa kama manamba mkuu, unaingia kazini wa kwanza na kutoka wa mwisho na ukiwa kazini hakuna ubosi wewe meneja ndiyo unaokuwa mstari wa mbele kufanya kazi mwanzo mwisho. Hayo ni maelezo kwa ufupi sana kutoka kwa vijana waliyobahatika kwenda huko kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Mfumo huu wa Israel ndiyo unaotumiwa na SUGECO katika utoaji wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo kwa vijana wetu wa Kitanzania.

Mapema mwezi wa kumi mwaka huu, SUGECO kwa kushirikiana na wizara ya kilimo kupitia iliyokuwa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) walifanikiwa  kuendesha mafunzo ya Mnyororo wa thamani wa Kuku na Sungura katika Kambi ya Vijana ya Kilimo  kwa Vitendo katika Kijiji Cha Mkongo wilayani Rufiji. Vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu walikuja kambini hapo kuhudhuria mafunzo hayo ambayo huendeshwa kwa muda  wa wiki mbili kwa kila darasa moja.

Kwa namna mafunzo hayo yalivyoratibiwa  na kuendeshwa kwa ustadi mkubwa, kila anayepita kambini hapo bila kujali kiwango chake cha elimu na umri, amekuwa akinolewa vizuri na kumwezesha kutoka na elimu itakayomfanya aweze kujitegemea yeye wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.

Hadi sasa ni awamu mbili tayari zimeshapita katika kambi hiyo ya vijana ya Mkongo Rufiji. Katika awamu ya pili ya mafunzo yaliyofanyika mwezi wa kumi, nami nilipata fursa ya kuwa mmoja wa wawezeshaji katika semina hiyo  na kupitia mafunzo hayo niliweza kuwafundisha vijana mnyororo mzima wa thamani wa kuku pamoja na Sungura.

Katika mafunzo hayo, kwahakika nimejionea kwa macho yangu ni kwa namna gani programu hii ya SUGECO inavyowanufaisha  Watanzania.
Kwakweli hizi ni aina ya programu ambazo kimsingi kama nchi tunapaswa kuziunga mkono ili Vijana wetu wapite katika kambi hizo ili waweze kujifunza kilimo kwa vitendo pamoja na stadi mbalimbali zinazotolewa katika kambi hiyo zenye lengo la kuwatengeza vijana wawe sababu ya kujiajiri wao wenyewe na kuajiri wengine.

Mfumo wetu wa elimu haumwezeshi moja kwa moja kijana kupata stadi zitakazomwezesha kujiajiri mwenyewe. Lazima vijana bila kujali kiwango chao cha elimu, wapatiwe aina hii ya mafunzo yanayotolewa na SUGECO ili kuwafanya vijana wetu watamani zaidi kujiajiri badala ya kusubiri ajira za Serikali au mashirika.

Nakumbuka katika mafunzo hayo mbali na kujifunza mnyoro wa thamani wa kuku na Sungura,  masomo yaliyoendeshwa kwa nadharia na vitendo, pia washiriki waliweza kujifunza kilimo cha mbogamboga na utengenezaji wa bidhaa mbalimba kama vile dawa za chooni, sabuni, shampoo, mishumaa, mafuta ya kupakaa ya mgando pamoja na nguo aina ya batiki.

Lakini somo jingine lililofundishwa siku hiyo ni somo la kubadilisha mtazamo wa kijana kutoka kwenye kasumba ya kutaka kuajiriwa na kupewa mbinu mpya  zitakazo msaidia kijana aweze kujiajiri wenyewe na kusimamia mradi wake kikamilifu.

Mkurugenzi wa SUGECO Bwana Revocatus Kimario wakati anatoa salamu zake za jioni kwa washiriki kabla ya kuwasilisha mada yake ya *Namna ya Kumuhudia Mteja,* alianza kwa nukuu ya mwalimu wa kubadilisha mtazamo wa vijana Mr Masimba *“a mindset changer”* iliyosema  “Tusaidiane kuondoa kutu vichwwani kwetu.” Nukuu hii ukiitafakari vizuri utaona ni kwa  namna gani ilivyojaa ukweli, vichwa vyetu vina kutu nyingi, tunahitaji kusaidiwa kuondolewa.

Bwana Kimario aliniendelea kuwatanabaisha vijana kwa kuwaambia kuwa “tukiwa hapa (kambini) degree zako zote tunaziweka pembeni kwasababu degree zako hazina maana sana kama hauna uwezo wa kutengeneza pesa.” Kimsingi Bwana Kimario alisisitiza sana ubunifu na kujiongeza. Katika hili alisema “aliyejaribu na akashindwa, anafaida kubwa kuliko asiyejaribu. Kufeli haina maana umeshindwa bali utatafuta namna nyingine ya kujaribu.”  Bwana Kimario katika kuongezea uzito hili,  alimnukuu Bwana Jeseph Chilton Pearce aliyeelezea thamani ya ubunifu aliyosema, to live a creative life we must lose our fear of being wrong.” Kwa taafsiri isiyo rasmi  akimaanisha kwamba kuishi maisha ya ubunifu kunahitaji kuondoa hofu ya kukosea.

Baada ya utangulizo huo aliyoutoa kwa washiriki, Mkurugenzi aliendelea na somo lake la *Namna ya Kumuhudumia Mteja.* Somo lilikuwa nzuri na kila mshiriki alivutiwa nalo. Laiti nafasi ingeruhusu ningeweza kulidadavua somo hilo kwa upana wake kadiri ya mafundisho yalivyotolewa Mkurugenzi ndugu  Kimario.

SUGECO imeundwa na vichwa vinavyojua kufikiria. Vinavyojua kiini cha tatizo la ajira kwa vijana na namna ya kuondoa tatizo hilo kupitia mafunzo ya kilimo Biashara. Kwahiyo wahenga walisema usione vyaelea, vimeundwa. Mambo yote mazuri yanayofanywa na SUGECO ni matokeo ya uratibu mzuri wa watu wafuatao: Kuna Dokta Anna Temu, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi na Dokta Flugence Mishili Makamu mwenyekiti. Kwenye kamati ya utalaam na ufundi kuna Dokta Daniel Ndyetabula, Dokta Betty Waized, na Dokta Felix Nandonde. Kwenye utawala utakutana na Bwana Revecatus Kimario, ambaye ni Mkurugenzi wa SUGECO, Bwana Joseph Masimba Mratibu wa Miradi, Bwana Ayubu E. Mundekesye meneja wa Mafunzo, Dickson Alex Mseko Meneja wa shamba na Prekseda Melkior kaimu meneja wa shamba.

Vichwa vyote hivyo kwa pamoja ndivyo vilivyotengeza wajasiriamali vijana wengi nchini katika sekta ya kilimo. Kila  kona ya nchi ukipita utakutana na vijana wengi waliyonolewa na SUGECO wakishughulika na mafundo mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kilimo. Kuna wale wanaolima alizeti na kuchakata mafuta, kuna wanaozalisha asali, kuna wanaolima mbogamboga kupitia shamba kitalu, kuna wanaozalisha mbegu za viazi lishe na kulima viazi. Kuna waliyosaidiwa kuanzisha viwanda mbalimbali vya usindikaji. Kuna wanao jishughulisha na ufugaji wa kuku, Samaki na Mifugo mingine. Ukipita SUGECO kwahakika lazima utabadilika kifikra na kimtazomo.

Kwa ajili ya kuwafikia vijana wengi nchini ilifaa sana kama Wizara ya Kilimo na Ushirika, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Vijana, kazi na ajira wangeangalia namna bora ya kushirikiana na SUGECO ili kuanzisha kambi mbalimbali za mafunzo ya kilimo kwa vitendo na kubadilisha fikra na mitazamo ya vijana. Kwa kufanya hivyo tutajenga taifa la kutenda badala ya kuwa taifa la kulalalamika. Na mwishowe matokeo chanya ya kiuchumi kwa vijana wetu na nchi kwa ujumla yangeonekana hasa katika kipindiki hiki ambacho nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Aman Ng'oma
Mkurugenzi  Mtendaji
Kinasoru East Africa Tanzania Ltd
Info@kinasoruea.co.tz or amanngoma@gmail.com
0767989713 or 0715989713
Nduka Street, Chamwino Bonanza
Dodoma
*TANZANIA.*

IPE THAMANI BIASHARA YAKO

Tafuta jina  zuri la biashara yako. Lisajili Brela. Kisha anza kulitumia. Na kama unaweza kusajili kampuni ni vyema ukafanya hivyo kwa kuwa ukiwa na kampuni utaweza kuaminiwa na watu wengi zaidi pamoja na taasisi mbalimbali.

Kusajili kampuni ni rahisi sana. Mahitaji yake ni kuwa na Memorandum of understand "MU" and article of association "AA" ambazo zote kwa pamoja zinakuwa kwenye kitabu kimoja.

MU yenyewe inaelezea zile shughuli zote ambazo kampuni yako itahitaji kuzifanya wakati AA kwa upande wake inaelezea siri za kampuni yaani nani ni nani ndani ya kampuni kwa maana ya uongozi, bodi ya wakurugenzi na hisa zao, mtaji anzia wa kampuni lakini pia namna ya mgao wa wanahisa ikitokea kampuni imekufa nk.

Kwa hiyo ukiwa na nyaraka hizo ni ruksa kwenda Brela kusajiliwa kampuni yako.

Ili kampuni yako iweze kusajiliwa inatakiwa iwe na board of directors kuanzia 2  hadi 50. Board of directors ndiyo wamiliki halali wa kampuni. Na sauti yao ndani ya kampuni inategemea sana kiasi cha hisa mwanabodi alichokiweka. Mwenye hisa kubwa ndiyo mwenye sauti zaidi ndani ya kampuni. Na hata kwenye kugawana faida mwenye hisa kubwa ndiye mwenye gawio kubwa.

Gharama za usajili wa kampuni inategemea na mtaji anzia wa kampuni husika. Kiwango cha chini kabisa ni mtaji wa kuanzia tsh 200,000/= na usiyozidi 1000,000/= ambapo ada yake ya usaji ni tsh 95,000/= wakati kiwango cha juu kabisa ni mtaji wa kuanzia tsh 50,000,000/= na kuendelea na ada yake ya usajili ni tsh 440,000/=

Kama utahitaji huduma ya kuongozwa kwenye usajili wa kampuni karibu tutakuongoza. Azimia kumiliki kampuni yako mwaka huu.

Aman Ng'oma
Kinasoru East Africa Tanzania Ltd
Info@kinasoruea.co.tz
0767989713
Dodoma

KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD

KARIBU KWENYE BLOG YETU YA KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD