Na Fadhy Mtanga
Jumanne, Disemba 10, 2013
Kwa Graça Machel na familia ya Mandela; kwa Rais Zuma na wajumbe wengine wa serikali; kwa wakuu wa nchi na serikali, waliopita na waliopo sasa, wageni wengine waalikwa – ni heshima ya kipekee mno kuwa nanyi leo, kusherehekea maisha yasiyo na kifani. Kwa watu wa Afrika Kusini – watu wa kila rangi na kila mfumo wa maisha – dunia inawashukuruni sana kwa kutushirikisha Nelson Mandela. Mapambano yake yalikuwa mapambano yenu. Shangwe yake ikawa shangwe yenu. Utu wenu na matumaini vilielezwa kupitia maisha yake, na uhuru wenu, na demokrasia yenu ni urithi wake uliotunzwa vema.
Ni vigumu kumsifu sana mtu yeyote – kuweza kudaka maneno na siyo matendo na nyakati zilizoyafanya maisha yake, lakini kupata ukweli muhimu umhusuo – furaha yake binafsi na huzuni; nyakati tulivu na ubora wa kipekee ulioiangaza nafsi ya mtu. Ni ngumu mno kwa gwiji katika historia, aliyelipeleka taifa katika haki, na katika mchakato uliowahuisha mabilioni ya watu ulimwenguni.
Aliyezaliwa wakati wa vita ya kwanza ya dunia, mbali kabisa kutoka mataifa yaliyokuwa na nguvu, mvulana mdogo aliyekuwa akichunga ng'ombe na kufundishwa na wazee wake wa kabila lake la Thembu – Madiba aliweza kuibuka kama mkombozi wa mwisho wa karne ya 20. Kama ilivyokuwa Ghandhi, aliongoza mapambano – harakati ambazo mwanzo wake ulionesha nuru ndogo ya mafanikio. Kama King, alipaza sauti yake ya manung'uniko ya wanaokandamizwa, na uadilifu muhimu wa haki kwa kila rangi. Alipambana na kifungo cha kikatili kilichoanza wakati wa Kennedy na Khrushchev, kilichokwenda hadi nyakati za mwisho za Vita Baridi. Aliibuka kutoka jela, pasipo kutumia nguvu ya bunduki, akaweza – kama Lincoln – kuileta nchi yake pamoja ilipokuwa katika hatari ya kuvunjika vipandevipande. Kama waasisi wa Amerika, aliweka misingi ya kikatiba ya kuhifadhi uhuru kwa ajili ya vizazi vijavyo – kujitolea kwa ajili ya demokrasia na utawala wa sheria ulioridhiwa si tu na uchaguzi uliomweka madarakani bali na hiyari yake ya kuachia madaraka.(P.T)
Kwa kuondoka kwake, na kwa mapenzi
aliyoyapata akiyastahili, inashawishi kumkumbuka kama alama, yenye
tabasamu na iliyotakata, iliyojiepusha na maovu ya wengine wasio na utu.
Lakini Madiba mwenyewe alikataa kwa nguvu zote taswira isiyo na maana.
Badala yake, alisisitiza katika kushiriki nasi mashaka yake na hofu
yake; makosa yake sambamba na kushinda kwake. "Mimi si mtakatifu,"
alisema, "isipokuwa kama mnanidhania mtakatifu mwenye dhambi asiyeacha
kujaribu."
Ni kwa sababu tu alikubali kuwa na
mapungufu – kwa kuwa alijaa ucheshi, hata kukosea, licha ya mizigo
mizito aliyokuwa ameibeba – nasi tukampenda vivyo hivyo. Hakuwa mtu
aliyetengenezwa kwa marumaru; alikuwa binadamu wa kawaida – mtoto na
mume, baba na rafiki. Hayo yote yanaonesha ni kwa nini tumejifunza mengi
sana kutoka kwake; na ndiyo sababu bado tuna mengi ya kujifunza kutoka
kwake. Kila alichokipata hakikuepukika. Katika utao wa maisha yake,
tunamwona mtu aliyeiweka nafasi yake kwenye historia kwa kupitia
mapambano na werevu; msimamo na imani. Ametuambia nini kinachowezekana
si tu kwa kupitia kurasa zenye vumbi za vitabu vya historia, bali pia
kwa kupitia maisha yetu wenyewe.
Mandela ametuonesha nguvu ya matendo,
kukabiliana na hatari kwa ajili ya ukamilifu wetu. Pengine, Madiba
alikuwa sahihi kusema amerithi, "ukaidi wa kujivunia, utukutu katika
haki" kutoka kwa baba yake. Kwa yakini ameshiriki na mamilioni ya
Waafrika Kusini weusi na wengine wa rangi mchanganyiko hasira ya
kuzaliwa katika "maelfu ya twezo, maelfu ya vitendo vilivyokosa utu,
maelfu ya nyakati zisizokumbukika.....matamanio ya kupambana na mfumo
uliowafunga watu wangu".
Lakini kama manguli wengine wa ANC –
akina Sisulu na akina Tambo – Madiba alikuwa na nidhamu ya hasira yake;
akayapeleka matamanio yake ya mapambano kitaasisi, na katika ulingo, na
kwa mikakati mahsusi, kwamba waume na wake wangeweza kusimama kwa ajili
ya utu wao. Vilevile, akayakubali madhara ya matendo yake, akifahamu
kuwa kusimamia haki na usawa kuna gharama zake. "Nimepambana dhidi ya
ukandamizaji wa watu weupe na nimepambana dhidi ya ukandamizaji wa watu
weusi," aliyasema hayo katika kesi yake ya mwaka 1964. "Nimeutukuza
ukamilifu wa demokrasia na jamii huru ambapo watu wote huishi kwa pamoja
katika maelewano na fursa sawa. Ni imani ninayoishi nayo nikitumaini
kuipata. Lakini ikihitajika, ni imani niliyojiandaa kuifia."
Mandela ametufundisha nguvu ya
matendo, lakini pia mawazo; umuhimu wa kuwa na sababu na hoja; umuhimu
wa kuwasoma siyo tu wale unaokubaliana nao, bali pia wale usiokubaliana
nao. Alifahamu mawazo hayawezi kuhifadhiwa ndani ya kuta za jela, ama
kuondoshwa kwa risasi ya mdunguaji. Akaigeuza kesi yake kuwa mashitaka
rasmi dhidi ya ubaguzi wa rangi kwa kupitia uzungumzaji wake na hisia
kali, pia kwa kupitia mafunzo yake kama wakili. Akaitumia miongo ndani
ya jela kunoa uwezo wake wa kujenga hoja, lakini pia kueneza kiu yake ya
maarifa kwa wengine katika harakati za mapambano. Akajifunza lugha na
tamaduni za wakandamizaji wake ili siku moja aweze kuwaonesha ni kwa
kiasi gani uhuru wao ulitegemea pia uhuru wake.
Mandela alionesha kuwa matendo na
mawazo pekee havitoshelezi; haijalishi ni sahihi kwa kiasi gani,
vinatakiwa kuwa kisheria na kitaasisi. Alikuwa mtu wa vitendo,
akazijaribu imani zake dhidi ya mazingira magumu na historia
iliyokuwepo. Katika kanuni ya msingi hakukubali kushindwa, hicho
kilipelekea akatae kuachiwa huru kwa masharti, akiukumbusha utawala wa
kibaguzi kuwa, "kamwe mfungwa haingii katika mikataba". Lakini alionesha
katika majadiliano magumu nia ya kupeana madaraka na kuandika sheria
mpya, hakuogopa kufikia maridhiano kwa malengo makubwa. Na kwa kuwa
hakuwa pekee yake kama kiongozi wa harakati, lakini akiwa mwanasiasa
mweledi, katiba iliyoandikwa ikawa yenye kuthamini demorasia ya rangi
tofauti; ikiweka bayana maono yake juu ya sheria inayolinda haki za
wachache na za wengi pia, na uhuru wa tunu kwa kila Mwafrika Kusini.
Hatimaye, Mandela alielewa juu ya
mambo yanayoiunganisha roho ya mwanadamu. Kuna neno Afrika Kusini –
Ubuntu – linaloelezea hiba yake kubwa: kutambua kwake kuwa sisi sote
tunaunganishwa katika namna mbalimbali ambazo zinaweza kutoonekana kwa
macho; ambazo zinaonesha u-moja kwa binadamu; kwamba tunakuwa sisi kwa
kushirikisha wengine katika u-sisi, na kuwajali wale wengine
wanaotuzunguka. Hatuwezi kufahamu ni kwa kiwango gani hii ilikuwa ndani
yake, ama kwa kiasi gani ilichochewa na kung'arishwa katika selo yenye
kiza na upweke. Lakini tunakumbuka ishara ya mwili wake, kwa ukubwa na
udogo wake – akiwatambulisha mabwana jela wake kama wageni wa heshima
siku aliyoapishwa; ndani ya sare ya Springbok; akiigeukia familia yake
akiihamasisha kupambana na VVU/UKIMWI – ikionesha kiwango cha juu cha
huruma yake na uelewa. Si tu alikolezwa na Ubuntu; bali aliwafundisha
wengi kuitafuta kweli ndani yao. Ilimchukua mtu kama Madiba kumkomboa si
tu mfungwa, bali na bwana jela pia; kuonesha kuwa unapaswa kuwaamini
wengine ili nao waweze kukuamini wewe; kufundisha kuwa maridhiano
hayamaanishi kuyadharau machungu yaliyopita, bali kumaanisha kupambana
nayo kwa ushirikishaji, ukarimu na ukweli. Alizibadili sheria, lakini na
mioyo pia.
Kwa watu wa Afrika Kusini, kwa wale
wote aliowapa msukumo kote ulimwenguni – kufariki kwa Madiba ni wakati
hasa wa maombolezo, na pia wakati wa kuyasherehekea maisha yake ya
kishujaa. Lakini ninaamini inapaswa pia kutupa wasaa wa kujitathimini
wenyewe. Kwa uaminifu, pasipo kujali mahali tulipo ama hali tulizo nazo,
shurti tujiulize: kwa namna gani ninayatekeleza mafunzo yake kwenye
maisha yangu mwenyewe?
Ni swali ninalojiuliza mwenyewe – kama
binadamu na kama rais. Tunafahamu kama ilivyo Afrika Kusini, Amerika
ililazimika kupambana na karne za ubaguzi wa rangi. Kama ukweli ulivyo
hapa, iliwachukua watu wasiohesabika kujitoa mhanga – wanaojulikana na
wasiojulikana – kuleta mapambazuko ya siku mpya. Michelle pamoja nami ni
wanufaishwa wa mapambano hayo. Lakini ndani ya Amerika na Afrika
Kusini, na nchi zingine kote ulimwenguni, hatuwezi kuruhusu maendeleo
yetu kuufunika ukweli kuwa kazi yetu haijafanywa. Mapambano yanayofuatia
ushindi juu ya usawa na haki za kiraia kote ulimwenguni yanaweza
yasitoshelezwe uadilifu na unyoofu ukilinganisha na yale yaliyotangulia,
lakini haimaanishi umuhimu kidogo. Kwa dunia ya leo, tungali tukiwaona
watoto wakiteswa na njaa, na magonjwa; kukosa shule, na matarajio yao
machache kwa maisha ya baadaye. Duniani kote leo, wake na waume wangali
wakifungwa kwa ajili ya imani zao kisiasa; na wangali wakiadhibiwa kwa
vile waonekanavyo, ama vile waabuduvyo, ama nani wawapendao.
Sisi, pia, lazima tutende kwa ajili ya
haki. Sisi, pia, lazima tutende kwa ajili ya amani. Wapo wengi mno
miongoni mwetu ambao kwa furaha tunaukumbatia urithi wa Madiba katika
maridhiano ya rangi, lakini kwa hisia kali tunayakataa mabadiliko ya
wastani ambayo yangeshindana na umasikini sugu na kukosekana kwa usawa
kunakokua. Wapo viongozi wengi mno wanaodai kushikamana na mapambano ya
uhuru ya Madiba, ilhali hawavumilii maoni tofauti kutoka kwa watu wao
wenyewe. Na wapo wengi wetu wanaosimama pembeni, wakistarehe katika
kuridhika ama wakizidharau sauti zetu zinapolazimika kusikika.
Maswali tunayokumbana nayo leo –
tukuze vipi usawa na haki; tuulinde vipi uhuru na haki za kibinadamu;
tukomeshe vipi migogoro na vita vya wenyewe – hayana majibu rahisi.
Lakini hakukuwa na majibu rahisi mbele ya mtoto yule pale Qunu. Nelson
Mandela anatukumbusha kuwa daima huonekana haiwezekani hadi jambo
linapotendwa. Afrika Kusini inatuonesha kuwa hivyo ni kweli. Afrika
Kusini inatuonesha tunaweza kubadilika. Tunaweza kuchagua kuishi katika
dunia isiyotafsiriwa kwa tofauti zetu, bali kwa matumaini yetu
yanayofanana. Tunaweza kuichagua dunia isiyotafsiriwa kwa mgogoro, bali
kwa amani na haki na fursa.
Hatutowaona watu kama Nelson Mandela
tena. Lakini wacha mimi niseme kwa vijana wadogo wa Afrika, na vijana
wadogo kote ulimwenguni – mnaweza kuyafanya maisha yake yakafanya kazi
ndani yenu. Zaidi ya miaka thelathini iliyopita, nikiwa bado mwanafunzi,
nilijifunza kuhusu Mandela na mapambano katika nchi yake. Ilichochea
kitu ndani yangu. Iliniamsha katika wajibu wangu – kwa wengine, na kwa
nafsi yangu -
- na kuniweka katika safari
isiyoyumkinika ambayo imenifikisha hapa leo. Na wakati sitoufikia mfano
wa Madiba, ananifanya nitake kuwa bora. Anazungumza kilicho bora ndani
yetu. Baada ya huyu mkombozi mufti kupumzishwa; baada ya sisi kurudi
kwenye majiji yetu na vijiji vyetu, na kurejea mizunguko yetu ya kila
siku, ni vema tuitafute nguvu yake – kwa ukuu wa roho yake – mahali
fulani ndani yetu. Na wakati giza likiingia usiku, wakati ukosefu wa
haki ukituelemea mioyoni mwetu, mikakati yetu kutofanikiwa – tumfikirie
Madiba, na maneno yaliyomletea faraja ndani ya kuta nne za selo yake:
Haijalishi namna mashaka yalivyoniandama,
Namna nilivyoshtakiwa na adhabu ndefu,
Mimi ndiye mwamuzi wa majaaliwa yangu,
Mimi ndiye nahodha wa nafsi yangu.
Ni nafsi kuu kwa kiasi gani.
Tutamkumbuka mno. Mwenyezi Mungu aibariki kumbukumbu ya Nelson Mandela.
Mwenyezi Mungu awabariki watu wa Afrika Kusini.
Imetafsiriwa katika Kiswahili na Fadhy Mtanga
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni