TASNIFU ZA NJANO5: KWA MASLAHI YA CHAMA, MH. MBOWE KIRI MAKOSA AU KANUSHA TUHUMA
CHUGUU LA ZAMANI:
Leo naomba kujadili umuhimu na ulazima wa uongozi wa CHADEMA chini ya
Mbowe kujibu hadharani hoja zao hao wanaoitwa wasaliti wa chama. Midhali
umma umezisikia hizo hoja hadharani basi kuna umuhimu na ulazima wa
uongozi kuzijibu kwa mifano na vielelezo hai ili kulinda na kutunza
heshima ya chama, lakini kubwa kwa uongozi huo kujisafisha kwa
wanaCHAMA.
MAYAI:
Kama kweli kuna wahafidhina na wabadhilifu ndani ya chama chetu, basi
kidogo kidogo hawa wafuasi wa wahafidhina na wabadhilifu wataelewa somo
na ipo siku watasema "tungejua.." lakini watakuwa wamechelewa kwani
nyota ya shamsi itakuwa inachomozea magharibi na kuzamia kaskazini,
naam, kitakuwa ni kipindi cha nakama na kila mtu akipambana kunusuru
nafsi yake bila kuzingatia maslahi mapana ya chama na taifa kwa ujumla
wake na ikifikia hapo CCM watatuimbia mapambio ya maombolezo tayari kwa
kuzikwa rasmi. Tandika majani blangeti udongo, mtenda mema kaenda.
Kama kweli kuna hao wahafidhina na wabadhilifu, niko na imani nia na
juhudi za Chacha Wangwe zingali zinaishi ndani yetu sisi vijana wachache
na ipo siku ndoto ya Chacha Wangwe itatimia kwa kuwa na CHADEMA kama
taasisi badala ya CHADEMA ya watu wachache wenye hulka za Panya na
Nyani. Panya tabia yake ni kung’ata huku anapuliza wakati Nyani hukiuka
sharia na kanuni za uendeshaji wa mahakama pindi akiletewa kesi ya
ngedere aliyeiba mahindi.
Watu wanahoji kamati kuu iliona makosa ya watu wa upande wa Zitto tu
na kuyajadili huko, lakini wale wote waliokuwa wanatumia mitandao
kumchafua Zitto na chama hawajaonwa na CC pamoja na kwamba watu hao
wanajulikana? Huu ni unyani, upanya nitaufafanua mbele.
Hatuwezi kushinda uchaguzi ujao wa 2015 kama uongozi wa sasa
hauaminiki pamoja na ushupavu wake. Ili tushinde uchaguzi ujao
tunatakiwa kuwa na uongozi shupavu, imara na wenye kuaminika. Uongozi wa
sasa inabidi uwe hivyo na uongozi ujao ni lazima uwe hivyo.
Lakini pia tunahitaji wanaCHAMA wasio ona soni kuukemea uongozi kama
ukipotoka, wanao amini juu ya misingi ya chama badala ya mtu na wanao
jitoa kwaajili taifa kwanza kabla ya chama; kwa kufanya hivi chama
kitaonekana kina wanaCHAMA wafia nchi na hivyo kuongeza mvuto kwa chama.
WanaCHAMA wasasa, hususani hawa wanao shinda humu kwenye mitandao
wanakubali kuimba wimbo wa usaliti bila kuutaka uongozi ujibu hoja za
hao wasaliti, yaani, wanajadili mtoa hoja badala ya kujadili hoja.
Mfano mwanaCHAMA anaweza kuhoji, hivi ni kweli chadema ina kamati ya
tenda? wajumbe wa hiyo kamati ni wakina nani? na kiongozi wa hiyo kamati
ni nani? ni kweli mwenyekiti wetu mbowe anaingilia kazi za kamati hii
kwaajili ya maslahi yake ya kibiashara? Hivi ni kweli hadi sasa mbowe
alichukua milioni 80 kwaajili ya kununua vifaa vya chama? Je kamati ya
tenda(kama ipo) inafanya kazi gani ikiwa Mbowe ndiye anayefanya kazi za
hiyo kamati? Hivi ni kweli hivyo vifaa hadi sasa havijafika? Kwanini
huku tukiendelea kuimba wimbo uliochuja wa usaliti tusimtake Mbowe ajibu
hoja hizi?
Pia hivi ni kweli kuwa hoja ya fedha kwenye kamati kuu ilikuwa
haijadiliwi hadi mwisho? Hivi pia ni kweli Mbowe huwa anakikopesha chama
bila maandishi na huja kujilipa kwa kiasi kikubwa kuliko hata kile
alichokikopesha chama? Nimesoma waraka wa Chacha Wangwe, hivi ni kwanini
Chacha aliitwa msaliti ikiwa hoja zake zilikuwa na mashiko na zenye
kuhitaji majibu? Kwanini kila anayemkosoa mbowe na kuhoji matumizi ya
chama huitwa msaliti? Hivi ni kweli mbowe hutumia mbinu ya kikoloni na
ya kiccm katika kupambana na wapinzani wake ndani ya chama? Kama sivyo
huu wimbo wa usaliti unalengo gani ikiwa wahusika wana hoja zenye lengo
la kujenga chama katika misingi ya kidemokrasia na uwazi?
Kitendo cha mtu kujifanya anakisaidia chama kifedha kwa kukikopesha
kisha anakuja kujilipa fedha nyingi kuliko hata deni lenyewe ni sawa na
kitendo cha kung’ata na kupuliza, huu ndio upanya wenyewe.
Uongozi wa sasa hauaminiki, pamoja na kwamba wakosoaji wake wamekiuka
katiba wakati wakifanya hivyo lakini bado kwa sisi ambao tuko nje ya
vikao vya maamuzi na ambao hizi tuhuma dhidi ya uongozi tumezisikia na
umma ambao hizi tuhuma umezisikia pia, ni vema uongozi ukazijibu
hadharani kwa mifano hai ili uongozi na chama kwa ujumla wake kipate
kuaminika kwa wanachama na umma ambao tunajua unahitaji chama makini na
chenye uwezo wa kujiongoza na kujisimamia kabla ya kupewa majukumu ya
kudhamini serikali.
MCHWA:
UONGOZI usipozijibu hizi tuhuma hadharani basi CHADEMA kitakuwa chama
hodari cha kulipua mabomu ya ufisadi na kwa vyovyote vile itaaminika
kuwa hayo mabomu ndio yaliyoipaisha CHADEMA na kuwa chama kikuu cha
upinzani na si uongozi imara, mzuri, na uwazi kama inavyoamika; Hapa
namaanisha(kama tuhuma zikithibiti) tumekuwa chama kikuu cha upinzani si
kwasababu uongozi wa Mbowe mzuri bali tumekuwa chama kikuu cha upinzani
kwasababu ya wabunge wetu tangu enzi ya Dr.Slaa wamekuwa wakifichua
MACHAFU na MADUDU ya serikali bila woga.
Uongozi mzuri na imara husimamia demokrasia ya ushindani, huwa na uwazi
katika matumizi yake ya fedha, mwenyekiti kama kiongozi mkuu haingilii
kazi za idara, mabaraza, kurugenzi na kamati za chama ambazo zimeundwa
kwa mujibu wa katiba.
KUMBIKUMBI:
Chini ya uongozi wa Mbowe demokrasia ilikanyagwa pale Zitto
alipoambiwa asigombee uenyekiti mwaka 2009, chini ya uongozi wa Mbowe,
Chacha Wangwe ameitwa msaliti kisa tu amehoji matumizi ya chama na
kitendo cha Mwenyekiti kukikopesha chama bila maandishi na kisha
kujilipa fedha nyingi, chini ya uongozi wa Mbowe, mwenyekiti wa chama
taifa anaingilia kazi za kamati ya tenda kwa kuchukua milioni 80 za
kununua vifaa vya chama na pia kujiingiza katika ununuzi wa magari na
pikipiki za chama ili hali ipo kamati yenye jukumu hilo.
Chini ya uongozi wa Mbowe tuna wanaCHAMA mashabiki wa watu na wengi
wao wamelipa ada ya uanachama kwa mwaka ule tu waliojiunga. Ziara za
kichama za viongozi wakuu na zile kazi za M4C zimezalisha mashabiki
wengi kuliko wanachama. Mfano Dr.Slaa alikuja huku Mikoa ya Kusini na
kufungua matawi na kusimamia uchaguzi wa matawi hayo.
Lakini alipoondoka yale matawi hayafanyi kazi na unaweza kusema kama
yamekufa na wale wanachama wameishia kuwa mashabiki wa Dr.Slaa. Sababu
Dr.Slaa alipoondoka huku nyuma hajaacha mtu wa kuwafundisha wale
wanaTAWI falsafa na itikadi ya chadema, wenye jukumu la kufundisha na
kutoa semina kwa wanaCHAMA wapya ni makatibu wa majimbo, wilaya na kata.
Makatibu hawa wanatumia muda mwingi kuganga njaa za kaya zao, hivyo
hawana muda wa kutosha wa kufanya kazi za chama. Hapa ndipo unapokuja
umuhimu wa makatibu wetu kulipwa mishahara au kupewa posho za kujikimu.
Tutaendelea kuimba wimbo wa kuacha ushabiki kwa watu lakini watu
wataendeleza ushabiki kama watu hao hawatufundishwa itikadi na falsafa
za chama chetu, mwanaCHAEMA mwenye kuijua itikadi na falsafa ya chadema
basi ataipenda chadema kwa kuzingatia itikadi na falsafa yake, mtu huyo
hatosubiria kugombea uongozi ndio alipe ada ya uanachama na hato
teteleka hata kama kiongozi mwandamizi na mwenye mvuto wa chama
akifukuzwa chamani.
Chini ya uongozi wa Mbowe vikao na maamuzi ya kamati kuu
hayaheshimiwi; kwa mfano iliamuliwa na kamati kuu hadi mwezi huu
uchaguzi wa ndani uwe umekwisha kamilika lakini ndio kwanza ratiba na
tarehe ya uchaguzi imetangazwa sasa tena mara baada ya yule ambaye aliye
semekana kuwa angegombea uenyekiti kupata majeraha ya kisiasa kutokana
na maamuzi ya kamati kuu, pia kuna fedha inasemeka kamati kuu iliazimia
zisiguswe lakini hizo fedha usalama wake uko shakani na kuna uwezekano
mkubwa chama kumpigia goti Mbowe kwaajili ya fedha za kugharamia
uchaguzi mkuu ujao.
Chini ya uongozi wa Mbowe kikao cha kamati kinatumika kama njia au kikao
cha kutekeleza mikakati ya Mbowe ya kuwadhibiti wapinzani wake wa
kisiasa ndani ya chama: rejea kutangazwa kwa tarehe na ratiba ya uchaguz
mara baada ya Zitto kuvuliwa nyadhifa zake na kuna kila dalili ya
mwanasiasa huyo kijana kufukuzwa kisa uenyekiti au kutamani vilaji vya
wakubwa. Chini ya uongozi wa Mbowe kila wanao hoji matumizi na kukosoa
uongozi huishia kuitwa wasaliti, wanatumiwa na CCM na TISS.
MALIKIA NA MUMEWE.
Kama kweli chini ya uongozi wa Mbowe hali ndani ya chama ndivyo ilivyo,
basi si kweli hata kidogo kuwa tumekuwa chama kikuu cha upinzani
kwasababu Mbowe ni kiongozi mzuri, bali tutakuwa tumekuwa chama kikuu
cha upinzani kwasababu wabunge wetu kazi zao kibunge ni nzuri na zenye
kumfikiria mlala hoi; hapa rejea kazi za kibunge za Dr.Slaa, Zitto,
Mnyika, Halima Mdee, Mch Msigwa. Hapa nimezingatia kazi zao kama
mawaziri vivuli na zile hoja binafsi walizoziwasilisha. Dr.Slaa EPA na
Zitto sakata la BUZWAGI zilipandisha chati ya CHADEMA.
Lakini pia tumekuwa chama kikuu cha upinzani kwasababu watanzania
wameshachoka siasa za Lipumba na Seif kujifanya wao ndio wenye uwezo wa
kuongoza kuliko mwanachama wowote wa CUF na pia watanzania wameshaichoka
CCM na MADUDU YAKE. Hivyo walipoona wabunge wetu wamefanya kazi nzuri
katika bunge la tisa kama wapinzani, wakaona CHADEMA ni chama cha kuweza
kuaminiwa uchaguzi unaofuata ambao ulikuwa ni wa 2010; imani yao
ikapelekea CHADEMA kuwa chama kikuu cha upinzani.
CHURA NA NYOKA.
Nimesema uongozi wa Mbowe ni imara lakini sasa hauaminiki,
sababu ya kutoaminika ni kutokana na tuhuma walizo ziibua wakosoaji wake
wa ndani ya chama. Kitendo cha uongozi wa chama kinachotaka kudhamini
serikali kushindwa kuaminika ni sawa na kumbikumbi waliojivunja mbawa
ili wajenge chuguu lao kuwa kivuno kwa chura kabla ya kukamilisha azima
yao, hii ni hatari kwa mustakabali wa kuzaliana na kuongezeka kwa mchwa.
CHUGUU JIPYA:
Yalopita si ndwele tugange yajayo, lakini pia hayo yaliyopita huwa ni
“ndwele” kama wahusika hawatakiri maovu waliyoyafanya aidha kwa bahati
mbaya au kwa kukusudia na kama hawata azimia kuyaacha sanjari na kujuta.
Au yaliyopita huwa “ndwele” endapo wahusika hawata yakanusha maovu
wanayo tuhumiwa kwa ushahidi uso kuwa na shaka yoyote.
Hivyo uongozi wa Mbowe unatakiwa kukiri makosa na kisha tusonge mbele
kiroho safi, au ukanushe tuhuma kwa ushahidi usio kuwa na shaka yoyote.
Ushahidi usiokuwa na shaka yoyote si lazima uthibitike mahakamani au
kwenye baraza la kusikiliza shauri, bali kwa watu waliokaa kwa nia njema
ya kujenga bila kigegezi huweza kuona ushahidi huo kwenye kikao chao na
kisha kuutangaza ili umma waujue.
Kwa kukiri makosa au kukanusha tuhuma kutarudisha imani ambayo sasa
imeshaanza kupotea, hivyo basi tutanza upya huku tukiendelea pale
tulipoishia kama chuguu jipya na imara lililojengwa mara baada ya
kumbikumbi wawili kuruka vihunzi vya nyoka, chura, binadamu, kuku na
kila aina ya hatari ambayo aghalabu huwakabili malikia na mfalme wa
kumbikumbi na mara baada ya kuvunja mbawa zao na kuanza kutembea ili
kupata eneo zuri tayari kwa kujenga chuguu.
Katika kulijenga chuguu letu liwe imara na kupunguza wanaCHAMA
mashabiki kwa watu, naamini program ya CHADEMA MSINGI itaondoa uanachama
wa ushabiki, lakini napendekeza makatibu wetu wa CHAMA, BAVICHA,
BAWACHA, na WAZEE ngazi ya kata ndio waaminiwe kwa program ya CHADEMA NI
MSINGI, hao ndio wapewe MAFUNZO na kisha kwa kushirikiana viongozi wa
matawi yaliyopo kwenye kata zao wataweza kutuletea MATOKEO MAZURI katika
program hii.
Pia matawi yetu ambayo yamepatiwa mafunzo ya CHADEMA MSINGI yafanye kazi
kama serikali kivuli kwenye mtaa wao kama mtaa wao unaongozwa na
mwenyekiti aliyetokana na CCM au wa chama kingine tafauti na CHADEMA,
kwani nina amini mafunzo hayo pia yatahusu umuhimu na ulazima wa
mwanaCHADEMA kushiriki katika kujiletea maendeleo katika mtaa anaoishi
na kusimamia rasilimali za mtaa zilizopo kwenye mtaa husika.
TANBIHI:
Lengo la makala hii ni kutaka uongozi wetu chini ya Mbowe kukiri makosa au kukanusha tuhuma na si lengo la makala hii kutuhumu na haipo hapa kutuhumu,
kwani naamini makosa kwa vingozi au/na tuhuma kwa viongozi hupunguza na
huchafua haiba njema ya chama kwa umma. Kukiri makosa au kukanusha
tuhuma hung’arisha haiba ya chama kwa umma.
Naomba niwaambie wanaCCM wanao chochea kuni kwa
haya yanayo tokea sasa ndani ya chama chetu, kwamba ninyi wanaCCM ni
kama wale walio lukumila uji wa mgonjwa asubuhi kwa kudhani mgonjwa
atakufa hatimaye kabla hata ya adhuhuri wakafa wenyewe. Nani asiyejua
kuwa kiza kikizidi ndio usiku wayoyoma? Nani asiyejua kuwa “kesho”
haijandikwa bali hutengenezwa na mja mwenyewe?
MUNGU IBARIKI CHADEMA NA VIONGOZI WAKE.
Njano5.
0655345394.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni