Jumamosi, 16 Juni 2018

UFUGAJI WA MBUZI NI UTAJIRI ULIYOJIFICHA

Mbuzi ni miongoni mwa wanyama wadogo wenye matumbo manne. Wanazaliana kwa haraka sana.  Kwa mwaka wana uwezo wa kuzaa mara mbili tofauti na ilivyo kwa Ng'ombe.

Toka ashike mimba hadi kuzaa hutumia siku 150 ambapo ni sawa na miezi 5. Baada ya kuzaa anakuwa na miezi miwili ya kunyonyesha kisha huachisha na kuwa tayari tena kupandwa na dume.

Mbuzi kwa mara ya kwanza huanza kupandwa na dume akiwa na umri wa miezi 9 hadi 12 kutegemeana na kosaafu, chakula anachokula na hali ya hewa.

Uwiano wa Dume na majike ni 1:25. Yaani kwenye kila majike 25 utahitaji dume 1.

Ukianza mradi  wako na  majike 100,  utahitaji madume 4.

Kwa hiyo ukiwa na mradi wa mbuzi 100 wenye umri wa kupandwa tayari, ndani ya miaka mitatu utakuwa mbali sana. Kwa mfano chukulia kila mbuzi azae mara mbili na kila mzao azae  mbuzi mmoja mmoja, siyo mapacha.  Ndani ya mwaka mmoja utakuwa na mbuzi 200, hivi ni vitoto. 

Kwahiyo kama mradi wako ulianza January na hapo hapo ukawapandisha, tunategemea mwezi wa tano watazaa. Watanyonyesha miezi miwili kwa maana wa sita na wa saba baada ya hapo ataacha kunyonyesha na kuwa tayari tena kupandwa.

Mwezi wa 12 watazaa kwa awamu ya pili na baada ya hapo kama kawaida watanyonyesha tena kwa miezi 2 kabla ya kuwaachisha.

Katika mbuzi watakaozaliwa tuchukulie kuwa nusu yao ni madume na 100 wengine ni majike. Kwahiyo yale madume 100 yote tutayaasi ili yaweze kukua haraka na vilivile kusaidia kuondoa harufu ya kibeberu na kufanya nyama iwe safi na kuwavutia walaji.

Mbuzi anakula nyasi pamoja na vichaka na hivyo kufanya ufugaji wake kuwa rahisi kitu cha msingi shamba liwe na maji pamoja na majani.

Ukiwa mvumilivu na ukawa makini kwenye usimamiaji wa mradi huu wa mbuzi, hakika matunda yake utayaona ndani muda mfupi sana.

Soko la mbuzi ni kubwa  na liko wazi. Kwa Dar es salaam soko la mbuzi liko kwenye mnada wa mbuzi wa Vingunguti na Pugu. Kwa Dodoma Soko la mbuzi liko kwenye minada ya Msalato, Kizota, Hombolo, Mpunguzi, Vikonje pamoja na machinjio ya kisasa ya TMC.

Kwa mikoani soko la Mbuzi liko minadani. Hata ukiwa na mbuzi wangapi ukiwapeleka tu mnadani utawauza wote na kwa bei na kwa bei ya ushindani. Lakini vilevile kama unaweza kuunda kampuni yako, unaweza  kusafirisha nyama ya mbuzi mwenyewe kwenda kwenye nchi za Dubai, Iraq, Kuweit, Oman na Falme za kiarabu. Vilevile unaweza kuwapeleka Somalia kama huogopi bunduki za Alshabab.

Hii ni fursa nyingine inayopaswa kumulikwa kwa upana wake. Tanzania tuna mapori mengi na yenye nyasi za kutosha na vichaka. Tuna mito mingi inayotiririsha maji mwaka mzima. Halikadhali kwa yale maeneo kame kama Dodoma na Singida bado yana fursa ya hazina kubwa ya maji chini. Ukiwa unaweza kumudu gharama za uchimbaji wa kisima bado utaweza kupata maji ya kutosha kwa ajili ya kunywesha mbuzi wako pamoja na kustawisha majini.

Utunzaji wa mbuzi si mgumu kama utafuata na kuzingatia kanuni bora za ufugaji.

Kwahiyo, kama ukiamua kufuga mbuzi basi utakuwa umechagua mradi usiyokuwa pasua kichwa.

Kinasoru East Africa imeanza kusambaza mbuzi chotara wenye kukua haraka, kustahimili magonjwa na kuendana na mazingira yetu ya Kitanzania. Kama unahitaji kuanzisha mradi huu,  tafadhili karibu tukushauri na vilevile tukuuzie mbegu bora za mbuzi chotara.

Uwekezaji katika ufugaji wa mbuzi huongeza utajiri kwa haraka.

Aman Ng'oma
Kinasoru East Africa Tanzania Ltd
Msalato Bible
Dodoma Tanzania.
0767989713/0715989713

Ijumaa, 12 Januari 2018

SUGECO IMEFUNGUA NJIA KWA VIJANA WAJASIRIAMALI KATIKA SEKTA YA KILIMO BIASHARA

Vijana wengi wa Tanzania tuna shida kubwa katika bongo zetu. Tumegeuka kuwa jamii ya kulaumu na kulalamika badala ya kuchukua hatua.Tunapenda urahisi. Tunasahau kuwa zama zimebadilika. Hatufikirishi vichwa vyetu kujaribu kutumia japo sehemu ndogo ya elimu tuliyoipata chuoni kutafuta fursa za kukamata.

Badala yake tumekaa tukibweteka tukiamini siku moja tutapata kazi ya ndoto zetu huku siku zikizidi kuyoyoma bila mafanikio. Tumekuwa mizigo kwa wazazi wetu badala ya kuwa msaada. Hakuna mawazo mapya tunayotoa. Zaidi tunatamani utanashati bila kuwa na pesa mfukoni. Kazi za kuchafuka hatuzitaki tena hata kama zinatengeneza pesa kiasi gani. Usomi wetu  umetufanya tuchague kazi.

Kijana asiyeenda shule,  unakuta ana uwezo mkubwa zaidi wa kutengeneza pesa,  kuliko msomi aliyehitimu chuo kikuu. Kijana asiyefika chuo kikuu hachagui kazi na vilevile yuko tayari kumtumia msomi kuuliza kitu asichokijua, lakini msomi yeye kwa upande wake hayuko tayari kujifunza kutoka kwa kijana asiyebahatika kufika chuo kikuu.

Tuna tatizo kubwa sana. Vijana wengi tumekosa mawazo mapya ya Ujasiriamali.  Bongo zetu zimelala. Hatuoni fursa mpya pamoja na kwamba fursa hizo zimejaa tele mtaani. Tunahitaji kufunguliwa vichwa vyetu na macho ili tuweza kuondolewa tongotongo zinazotufanya tushishindwe kuona fursa.

Changamoto ya kushindwa kuona fursa  haiwakabili tu vijana wasomi waliyohitimu vyuo mbalimbali pekee yao bali hata wazee wetu waliyostaafu kutoka kwenye utumishi wa umma au sekta binafsi nao wanakabiliwa na tatizo hili.

Utastaajabu kumwona mstaafu namna anavyohangaika mtaani kuyakabili maisha yake mapya. Hawezi kufanya kazi nyingine zilizo nje ya fani yake. Matokeo yake baada ya kustaafu utumishi wake,  anakuwa hana uwezo tena wa kuratibu na kusimamia mradi utakaompatia pesa na kumwezesha kuishi maisha yanayofanana na yale aliyokuwa akiyaishi alipokuwa kazini.

Mstaafu anaishi maisha ya ajabu kabisa pamoja na kwamba,  alipatiwa mafao yake yote na mfuko wake wa hifadhi ya jamii. Amekosa elimu ya ujasiriamali. Pesa za mafao yake ya kustastaafu,  anaingiza kwenye miradi mfu. Matokeo yake anapata anguko kubwa lisilo kuwa na mfano.

Lakini yote hii ni kwa sababu kulikuwa hakuna taasisi au watu waliyojitoa sawasawa kunoa bongo za watu wengine ili wawe na uwezo kujitegemea mara baada ya kustaafu au kumaliza viwango mbalimbali vya elimu.

Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO),  kwa upande wao waliliona hili na kuamua kwadhati kabisa kujitoa kuwasaidia wahitimu wa vyuo mbalimbali na vijana wasiyowahitimu ili waweze kujiajiri wao wenyewe katika sekta ya Kilimo Biashara.

Kupitia SUGECO, vijana wamekuwa wakifundishwa stadi mbalimbali za kilimo biashara ikiwemo mbinu bora za kuendesha kilimo cha kisasa, kilimo chenye tija, ufugaji bora,  Uongezaji wa thamani wa mazao ya Kilimo na mifugo, Usindikaji wa bidhaa mbalimbali za kilimo, uendeshaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo na kuondoa tongotongo katika bongo za vijana, kuwawezesha vijana wahitimu wa vyuo kuwa na miradi yao binafsi na kupata fursa ya kusimamiwa kwa ukaribu na hatua kwa hatua hadi mradi utakaposimama.

Si hivyo tu bali pia SUGECO wanajishughulisha na utoaji wa ufadhili wa mashamba Kitalu au Greenhouse kama ilivyozoeleka  na wengi  kwa vijana ili kuwawezesha  kuendesha shughuli za kilimo chenye udhibiti wa magonjwa. Kana kwamba haitoshi,   SUGECO wanaendesha programu kabambe ya kuwapeleka vijana nchini Israel kushiriki mafunzo kwa vitendo katika sekta ya Kilimo. Kila mwaka kuna kundi la vijana wasiyopungua 30 wanapelekwa Israel.

Ukikaa na vijana waliyopata fursa ya kwenda nchini Israel na ukasikiliza shuhuda zao, utabaini wazi kuwa sisi watanzaia bado hatufanyi kazi kabisa. Tunapoteza  muda wetu mwingi  kizembezembe.  Wenzetu kule wanachunga sana muda wao na kujali zaidi kazi. Kwao siku zote muda huwa huwatoshi kutekeleza majukumu yao,  hivyo wanajitahidi kuitumia kila dakika inayopatikana kufanya kitu kinachoonekana. Muda kwao una thamani kubwa sana hivyo haupaswi kuchezewa hata kidogo.

Siku zote waisrael  wanaamini kuwa hakuna mtu atakayekufa kwa kufanya kazi. Kwa hiyo ukiwa Israel masaa mengi utayatumia kwa ajili ya kufanya kazi. Siku ya mapumziko kwao ni siku moja tu katika wiki na ni siku ya jumamosi ambayo pia siku hiyo wanaitumia kwa ajili ya kukufanya Ibada.

Kuwa meneja Israel ni tofauti sana na kuwa meneja katika nchi zetu za afrika ambapo meneja anakuwa anaongoza kwa  kula bata,  kule ukiwa meneja hakuna kula bata, bali  meneja unakuwa kama manamba mkuu, unaingia kazini wa kwanza na kutoka wa mwisho na ukiwa kazini hakuna ubosi wewe meneja ndiyo unaokuwa mstari wa mbele kufanya kazi mwanzo mwisho. Hayo ni maelezo kwa ufupi sana kutoka kwa vijana waliyobahatika kwenda huko kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo. Mfumo huu wa Israel ndiyo unaotumiwa na SUGECO katika utoaji wa mafunzo ya kilimo kwa vitendo kwa vijana wetu wa Kitanzania.

Mapema mwezi wa kumi mwaka huu, SUGECO kwa kushirikiana na wizara ya kilimo kupitia iliyokuwa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) walifanikiwa  kuendesha mafunzo ya Mnyororo wa thamani wa Kuku na Sungura katika Kambi ya Vijana ya Kilimo  kwa Vitendo katika Kijiji Cha Mkongo wilayani Rufiji. Vijana kutoka maeneo mbalimbali ya nchi yetu walikuja kambini hapo kuhudhuria mafunzo hayo ambayo huendeshwa kwa muda  wa wiki mbili kwa kila darasa moja.

Kwa namna mafunzo hayo yalivyoratibiwa  na kuendeshwa kwa ustadi mkubwa, kila anayepita kambini hapo bila kujali kiwango chake cha elimu na umri, amekuwa akinolewa vizuri na kumwezesha kutoka na elimu itakayomfanya aweze kujitegemea yeye wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.

Hadi sasa ni awamu mbili tayari zimeshapita katika kambi hiyo ya vijana ya Mkongo Rufiji. Katika awamu ya pili ya mafunzo yaliyofanyika mwezi wa kumi, nami nilipata fursa ya kuwa mmoja wa wawezeshaji katika semina hiyo  na kupitia mafunzo hayo niliweza kuwafundisha vijana mnyororo mzima wa thamani wa kuku pamoja na Sungura.

Katika mafunzo hayo, kwahakika nimejionea kwa macho yangu ni kwa namna gani programu hii ya SUGECO inavyowanufaisha  Watanzania.
Kwakweli hizi ni aina ya programu ambazo kimsingi kama nchi tunapaswa kuziunga mkono ili Vijana wetu wapite katika kambi hizo ili waweze kujifunza kilimo kwa vitendo pamoja na stadi mbalimbali zinazotolewa katika kambi hiyo zenye lengo la kuwatengeza vijana wawe sababu ya kujiajiri wao wenyewe na kuajiri wengine.

Mfumo wetu wa elimu haumwezeshi moja kwa moja kijana kupata stadi zitakazomwezesha kujiajiri mwenyewe. Lazima vijana bila kujali kiwango chao cha elimu, wapatiwe aina hii ya mafunzo yanayotolewa na SUGECO ili kuwafanya vijana wetu watamani zaidi kujiajiri badala ya kusubiri ajira za Serikali au mashirika.

Nakumbuka katika mafunzo hayo mbali na kujifunza mnyoro wa thamani wa kuku na Sungura,  masomo yaliyoendeshwa kwa nadharia na vitendo, pia washiriki waliweza kujifunza kilimo cha mbogamboga na utengenezaji wa bidhaa mbalimba kama vile dawa za chooni, sabuni, shampoo, mishumaa, mafuta ya kupakaa ya mgando pamoja na nguo aina ya batiki.

Lakini somo jingine lililofundishwa siku hiyo ni somo la kubadilisha mtazamo wa kijana kutoka kwenye kasumba ya kutaka kuajiriwa na kupewa mbinu mpya  zitakazo msaidia kijana aweze kujiajiri wenyewe na kusimamia mradi wake kikamilifu.

Mkurugenzi wa SUGECO Bwana Revocatus Kimario wakati anatoa salamu zake za jioni kwa washiriki kabla ya kuwasilisha mada yake ya *Namna ya Kumuhudia Mteja,* alianza kwa nukuu ya mwalimu wa kubadilisha mtazamo wa vijana Mr Masimba *“a mindset changer”* iliyosema  “Tusaidiane kuondoa kutu vichwwani kwetu.” Nukuu hii ukiitafakari vizuri utaona ni kwa  namna gani ilivyojaa ukweli, vichwa vyetu vina kutu nyingi, tunahitaji kusaidiwa kuondolewa.

Bwana Kimario aliniendelea kuwatanabaisha vijana kwa kuwaambia kuwa “tukiwa hapa (kambini) degree zako zote tunaziweka pembeni kwasababu degree zako hazina maana sana kama hauna uwezo wa kutengeneza pesa.” Kimsingi Bwana Kimario alisisitiza sana ubunifu na kujiongeza. Katika hili alisema “aliyejaribu na akashindwa, anafaida kubwa kuliko asiyejaribu. Kufeli haina maana umeshindwa bali utatafuta namna nyingine ya kujaribu.”  Bwana Kimario katika kuongezea uzito hili,  alimnukuu Bwana Jeseph Chilton Pearce aliyeelezea thamani ya ubunifu aliyosema, to live a creative life we must lose our fear of being wrong.” Kwa taafsiri isiyo rasmi  akimaanisha kwamba kuishi maisha ya ubunifu kunahitaji kuondoa hofu ya kukosea.

Baada ya utangulizo huo aliyoutoa kwa washiriki, Mkurugenzi aliendelea na somo lake la *Namna ya Kumuhudumia Mteja.* Somo lilikuwa nzuri na kila mshiriki alivutiwa nalo. Laiti nafasi ingeruhusu ningeweza kulidadavua somo hilo kwa upana wake kadiri ya mafundisho yalivyotolewa Mkurugenzi ndugu  Kimario.

SUGECO imeundwa na vichwa vinavyojua kufikiria. Vinavyojua kiini cha tatizo la ajira kwa vijana na namna ya kuondoa tatizo hilo kupitia mafunzo ya kilimo Biashara. Kwahiyo wahenga walisema usione vyaelea, vimeundwa. Mambo yote mazuri yanayofanywa na SUGECO ni matokeo ya uratibu mzuri wa watu wafuatao: Kuna Dokta Anna Temu, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi na Dokta Flugence Mishili Makamu mwenyekiti. Kwenye kamati ya utalaam na ufundi kuna Dokta Daniel Ndyetabula, Dokta Betty Waized, na Dokta Felix Nandonde. Kwenye utawala utakutana na Bwana Revecatus Kimario, ambaye ni Mkurugenzi wa SUGECO, Bwana Joseph Masimba Mratibu wa Miradi, Bwana Ayubu E. Mundekesye meneja wa Mafunzo, Dickson Alex Mseko Meneja wa shamba na Prekseda Melkior kaimu meneja wa shamba.

Vichwa vyote hivyo kwa pamoja ndivyo vilivyotengeza wajasiriamali vijana wengi nchini katika sekta ya kilimo. Kila  kona ya nchi ukipita utakutana na vijana wengi waliyonolewa na SUGECO wakishughulika na mafundo mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa kilimo. Kuna wale wanaolima alizeti na kuchakata mafuta, kuna wanaozalisha asali, kuna wanaolima mbogamboga kupitia shamba kitalu, kuna wanaozalisha mbegu za viazi lishe na kulima viazi. Kuna waliyosaidiwa kuanzisha viwanda mbalimbali vya usindikaji. Kuna wanao jishughulisha na ufugaji wa kuku, Samaki na Mifugo mingine. Ukipita SUGECO kwahakika lazima utabadilika kifikra na kimtazomo.

Kwa ajili ya kuwafikia vijana wengi nchini ilifaa sana kama Wizara ya Kilimo na Ushirika, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Vijana, kazi na ajira wangeangalia namna bora ya kushirikiana na SUGECO ili kuanzisha kambi mbalimbali za mafunzo ya kilimo kwa vitendo na kubadilisha fikra na mitazamo ya vijana. Kwa kufanya hivyo tutajenga taifa la kutenda badala ya kuwa taifa la kulalalamika. Na mwishowe matokeo chanya ya kiuchumi kwa vijana wetu na nchi kwa ujumla yangeonekana hasa katika kipindiki hiki ambacho nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda.

Aman Ng'oma
Mkurugenzi  Mtendaji
Kinasoru East Africa Tanzania Ltd
Info@kinasoruea.co.tz or amanngoma@gmail.com
0767989713 or 0715989713
Nduka Street, Chamwino Bonanza
Dodoma
*TANZANIA.*

IPE THAMANI BIASHARA YAKO

Tafuta jina  zuri la biashara yako. Lisajili Brela. Kisha anza kulitumia. Na kama unaweza kusajili kampuni ni vyema ukafanya hivyo kwa kuwa ukiwa na kampuni utaweza kuaminiwa na watu wengi zaidi pamoja na taasisi mbalimbali.

Kusajili kampuni ni rahisi sana. Mahitaji yake ni kuwa na Memorandum of understand "MU" and article of association "AA" ambazo zote kwa pamoja zinakuwa kwenye kitabu kimoja.

MU yenyewe inaelezea zile shughuli zote ambazo kampuni yako itahitaji kuzifanya wakati AA kwa upande wake inaelezea siri za kampuni yaani nani ni nani ndani ya kampuni kwa maana ya uongozi, bodi ya wakurugenzi na hisa zao, mtaji anzia wa kampuni lakini pia namna ya mgao wa wanahisa ikitokea kampuni imekufa nk.

Kwa hiyo ukiwa na nyaraka hizo ni ruksa kwenda Brela kusajiliwa kampuni yako.

Ili kampuni yako iweze kusajiliwa inatakiwa iwe na board of directors kuanzia 2  hadi 50. Board of directors ndiyo wamiliki halali wa kampuni. Na sauti yao ndani ya kampuni inategemea sana kiasi cha hisa mwanabodi alichokiweka. Mwenye hisa kubwa ndiyo mwenye sauti zaidi ndani ya kampuni. Na hata kwenye kugawana faida mwenye hisa kubwa ndiye mwenye gawio kubwa.

Gharama za usajili wa kampuni inategemea na mtaji anzia wa kampuni husika. Kiwango cha chini kabisa ni mtaji wa kuanzia tsh 200,000/= na usiyozidi 1000,000/= ambapo ada yake ya usaji ni tsh 95,000/= wakati kiwango cha juu kabisa ni mtaji wa kuanzia tsh 50,000,000/= na kuendelea na ada yake ya usajili ni tsh 440,000/=

Kama utahitaji huduma ya kuongozwa kwenye usajili wa kampuni karibu tutakuongoza. Azimia kumiliki kampuni yako mwaka huu.

Aman Ng'oma
Kinasoru East Africa Tanzania Ltd
Info@kinasoruea.co.tz
0767989713
Dodoma

Jumamosi, 30 Desemba 2017

UFUGAJI WA BROILERS

Broilers ni kuku wa nyama ambao hufugwa kwa muda wa wiki nne hadi tano kutegemeana na matunzo na kuwa tayari kwenda sokoni. Ufugaji wa broilers mara nyingi hutumiwa kama njia rahisi ya kumwongezea mfugaji mtaji wa haraka.

Watu wengi wanapenda kufuga kuku aina ya broilers lakini wanapata changamoto kubwa  katika kufanya makadirio ya gharama za ufugaji zinazohitajika.

Kwa kuzingatia umuhimu huu kwa wafugaji, nimeona niwatengenezee mwongozo wa bajeti ambayo mfugaji ataweza kuitumia kama kiongozi wake  pale atakapohitaji kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku wa nyama aina hii ya Broilers.

Asante

Aman Ng'oma
Dodoma
0767989713

RUVUMA NI LULU YA NCHI YETU

Tupambane tuijenge Ruvuma yetu. Tuweke kando itikadi zetu tuungane tuwe kitu kimoja.  Tuaminiane tufanye kazi. Wenzetu mliyopata bahati ya kuwa kwenye vyombo vya maamuzi basi mjitahidi kuwa wazalendo kwa ajili ya mkoa wetu. Ni aibu kubwa kuona kila kitu hakiendi. Mkoa unadorola.

Tulipata fungu la kuboresha barabara za mitaa ya Songea Mjini lakini cha kushangaza hata kuwasimamia makadarasi tuliyowapa kazi wenyewe  tulishindwa hadi Mkuu wa mkoa mpya,  Mama Mndeme amekuja kuwatimua. Madiwani tuliyowachagua wapo tu wanatazama,  hawajui hata wajibu wao. Mkuu wa mkoa mpya asingekuja maana yake  uozo huo usingeonekana!

Watu waliyopewa dhamana hawawajibiki ipasavyo. Tunapaswa kuwa kitu kimoja na tuzungumze lugha moja. Tukiondoa maslahi binafsi na tukatanguliza mbele maslahi ya mkoa wetu
kwa kila Mwanaruvuma kwa nafasi aliyonayo,  naamini vizazi vyetu vijavyo vitatukumbuka kwa maamuzi mazuri tunayoyafanya sasa.

Ruvuma ni lulu  ya nchi. Tena ni lulu kwelikweli.  Taifa linaitegemea kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kutokana na kuwa na hali ya hewa nzuri, hali ya hewa inayoruhusu uzalishaji wa mazao mbalimbali, uchapakazi wa wananchi wetu unaosukumwa kutoka ndani ya mioyo yao unaongeza chachu ya ukuaji  wa kilimo.  Ndiyo maana siku zote wananchi wa Ruvuma huwezi kuwasikia wakilia njaa, bali  utakachowasikia wakilia ni kukosa masoko ya uhakika  kwaajili ya kuuza mazao yao. Mwana Ruvuma humtumi kazi, kufanyakazi ni jadi yake. Ndiyo maana hata sera ya Rais wetu Dokta John Pombe Magufuli ya hapa kazi tu haimpi tabu mwananchi yoyote wa Mkoa wa Ruvuma kwani wamezoea Kufanya kazi.

Ruvuma imebarikiwa hasa na Mwenyezi Mungu. Tuna utajiri mkubwa wa madini kuanzia Makaa ya Mawe kule Mbinga, madini ya Urani kule Namtumbo nk. Naamini kama Serikali itaamua kwa dhati kabisa kuwekeza kwenye tafiti za madini na rasilimali nyinginezo za ardhini, bila shaka tutashangwazwa na utajiri utakaoibuliwa. Ruvuma ina kila kitu.

Kinachotakiwa kufanywa ni kuhakikisha kuwa watu wa mipango miji wa mkoa wa Ruvuma wanatengeneza  mazingira  yatakayovutia uwekezaji mkoani kwetu. Kazi kubwa ni kutengeneza mazingira tu,  Wawekezaji wako wengi sana, wakiona mazingira yako vizuri watakuja tena kwa kukimbia. Ni sisi tu tunapaswa kujua namna ya kuwatengenezea mazingira rafiki na kuwahakikishia usalama wa mitaji yao watakayoiwekeza.

Maeneo ya uwekezaji ni mengi, kuna kilimo, Supermarkets,  MALL za biashara, Mahotel makubwa, Vitega uchumi, Mabustani ya kupumzikia, Maviwanda makubwa ya kuzalisha na kusindika bidhaa mbalimbali, Uwekezaji katika sekta ya Utalii nk

Kufanikisha hili ni muhimu  miundombinu ya mjini hasa barabara za mitaa  zikatengenezwa vizuri huku pembeni ziking'arishwa kwa taa za barabarani. Kila kitu kinawezekana ni mipango tu.

Kwa sasa nina imani kubwa na mkuu wetu mpya wa mkoa Mama Mndeme, naamini kupitia yeye atatuvusha na  tutafika salama tunakoenda ila kitu cha muhimu, madiwani wetu  wanapaswa kutambua wajibu waliyonao kwa mustakabali wa maendeleo ya mkoa wetu. Wao ndiyo wasimamizi wakubwa wa miradi yote ya maendeleo ya mkoa. Wao wakilala wajue kila kitu kimelala. Watu wamekalia makundi yasiyokuwa na msingi wowote badala ya kuangalia ni namna gani Ruvuma itaendelea. Pongezi kubwa kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassimu Majliwa Kassimu kwa kuona tofauti za madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Huu ni mfano tu ambao hata halmashauri nyingine za mkoa wa Ruvuma zikimulikwa lazima utakutana na tofauti hizi za maslahi binafsi zikiwa zimetamalaki.

Serikali yetu imejitahidi kuufungua Mkoa wetu wa Ruvuma kwa barabara za lami na kwa sasa tunaletewa mradi mkubwa wa grid ya taifa ya umeme,  tunashukuru kupitia mradi huu,  vijiji vingi vya mkoa vimeweza kunufaika. Kukamilika kwa mradi wa REA, ni ishara tosha ya mwanzo mpya wa maendeleo endelevu mkoani kwetu.

Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa jitahada kubwa inayoifanya ya kuufungua mkoa wetu wa Ruvuma hasa kwenye upande wa Miundombinu. Hali sasa imeimarika sana ukilinganisha na siku za nyuma. Hatahivyo,  bado tunaendelea kutoa maombi kwa Setikali yetu dhidi ya barabara kuu ya Njombe hadi Songea Mjini. Tunatamani na yenyewe iweze kutazamwa kwa jicho la kipekee. Barabara  imekuwa finyu na imechoka ile mbaya. Barabara  toka enzi ya mkoloni hadi leo bado iko vilevile, kwakweli inahitaji kutafutiwa fungu mahsusi ili ijengwe upya na ilete sura mpya. Naamini kama itajengwa upya hata ajali zitapungua sana hasa kwa kuzingatia hatari ya barabara yenyewe ilivyo.

Nawasilisha

Aman Ng'oma
*Mkereketwa wa Maendeleo Ruvuma*





Jumatano, 29 Machi 2017

Dkt. JOHANSEIN RUTAIHWA: KIATU CHA UBUNGE WA AFRIKA MASHARIKI KINANITOSHA, NIVALISHENI NIWATUMIKIE



Nafasi ya ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni sehemu mojawapo ambayo nchi inapata wawakilishi wake katika Jumuiya hiyo ukiachana  na nafasi ya ajira za moja kwa moja zitolewazo na Jumuiya hii. Ni sehemu nyeti sana kwa nchi katika kupata watetezi kwenye masuala yanayohusu nchi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hawa ni wawakilishi wetu hatupaswi kufany makosa kwenye teuzi zao, tunapaswa  tuchague watu makini wenye uwezo wa kuliwakilisha vyema taifa letu. Hatutakiwi kuruhusu nchi yetu imezwe na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki. Mchango na umuhimu wa Tanzania kwenye nchi za Afrika Mashariki, kati na Afrika kwa ujumla wake lazima ubaki pale pale kama ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere. Tunataka Tanzania iwe kigezo kwenye nyanja zote kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kijamii. Maslahi ya Taifa kimataifa yanategemea zaidi uwezo wetu wa kushawishi.
Kutokana na umuhimu huo kwa taifa, tunahitaji wawakilishi wanaojiweza katika kushawishi, wanaojua historia yetu, vipaumbale vyetu lakini vilevile wanaofahamu vyema lugha ya kingereza ambayo ndiyo lugha rasmi ya mawasiliano ndani ya jumuiya hiyo. Kwahiyo tunapotafuta wawakilishi lazima tuangalie ujuzi wao kwenye kuzungumza lugha ya kiingereza na uwezo wao wa kushawishi kupitia ujenzi wa hoja madhubuti zenye uzito na mashiko.

NAONA LUGHA GONGANA KATIKA UJENZI WA MNARA WA BABERI

Nakumbuka siku za nyuma Chama cha Mapinduzi CCM kilielemewa sana na upinzani wakati wa katibu mkuu mzee wetu Yusuph Makamba na baadae Bwana Wilson Mkama. Upinzani ulishika hatamu, kila kona walitawala wao kuanzia kwenye vyombo mbalimbali vya habari, mitaani, kwenye vijiwe vya kahawa na hadi maofisini. Kila siku hoja nzito zilikuwa zikiibuliwa na upinzani, hoja za kukidhoofisha Chama na Serikali yake hasa kwenye mambo ya ufisadi.
Mabadiliko ya Sekretarieti kutoka ya Yusuph Makamba hadi ya Mheshimiwa Abdurahamani Kinana, kama katibu mkuu wa chama, Philip Mangula, kama makamu mwenyekiti huku Mheshimiwa Nape Nnauye, akiwa kama katibu Mwenezi wa Chama kulileta fikra na mawazo mapya ya kuendesha chama. Nadhani kila mtu anakumbuka kazi iliyofanywa na Sekretarieti hiyo katika kurudisha uhai wa chama. Mheshimiwa Kinana yeye kwa upande wake alizunguka nchi nzima kufufua chama na kuleta matumaini mapya kwa wanachi huku Bwana Nape Nnauye yeye kwa upande wake alikuwa shupavu na shapu kujipu hoja yoyote inayotolewa na upinzani na kuitolea ufafanuzi wa kina. Kwahakika wapinzani walimgwaya ile mbaya bwana Nape Nnauye na mara nyingi walipokuwa wakishindwa kujibu hoja zake waliishia tu kumwita mlopokaji lakini kimsingi kama katibu mwenezi aliweza kusimama katika nafasi yake vizuri na kukiweka chama katika uimara ambao umesaidia hata kukivusha vyema chama hicho katika kipindi cha uchaguzi uliyopita, uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa kuwahi kutokea katika historia ya siasa za vyama vingi nchini Tanzania tangu kuasisiwa kwake mwaka 1992. Katika uchaguzi huo kama kusingelikuwa na Sekretarieti imara naamini leo hii tungelisema mambo mengine juu ya uhai wa Chama cha Mapinduzi.
Lakini leo hii asubuhi nimesikia Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri na katika mabadiliko hayo Mheshimiwa Prof. Palamagamba Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na sheria wakati Dkt. Harrison Mwakyembe amechukua nafasi ya Mheshimiwa Nape Nnauye katika nafasi ya Uwaziri wa Habari, Michezo na Utamaduni. Ni kweli ni uamuzi wa Rais kufanya mabadiliko kadili ya matakwa yake na hakuna wa kumpangia. Na mamlaka haya amepewa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi. Lakini ni muhimu kutambua mchango wa mtu katika chama na nchi. Nape Nnauye ni kijana anayehitaji kufunzwa pale anapokosea kama kijana. Kumwajibisha kama ilivyotokea sioni kama kutasaidia kuimarisha chama na kuleta mustakabari bora wa nchi. Nilidhani kama kuna kutofautiana kidogo ni muhimu zaidi kutumia vikao kumaliza tofauti hizo. Wahenga walisema Mnyonge Mnyongeni lakini haki yake mpeni. Nape Nnauye ni kijana chapakazi haswa asiyekubali kunyamaza pale anapoona kwenye mamlaka yake kuna jambo limetokea. Ni mwepesi kupaza sauti ili kutolea ufafanuzi hasa yale masuala yenye kuzua taharuki.
Kitu ninachokiona kwa sasa katika chama cha Mapinduzi chama kongwe nchini na bara la Afrika kwa ujumla wake ni kama kuna lugha gongana katika ujenzi wa mnara wa Baberi. Na nadhani matokeo ya lugha gongana katika ujenzi wa mnara ule wote tunajua kama ulivyoanishwa katika vitabu vitakatifu. Ni muhimu kama chama kinachoongoza dola kuwa makini katika maamuzi yanayochukuliwa vinginevyo tutakuja kujilaumu wenyewe kwa makosa madogo ya kimkakati tunayoyafanya. Kama mtu atajaribu kutatazama mgongoro huu kwa jicho la tatu, anaweza kubaini dhahiri kuwa kama kuna ugomvi wa kugombea fito katika ujenzi wa nyumba kitu ambacho kama haitachukuliwa hatua za haraka kutatua tatizo, huwenda ikaleta madhara makubwa kwa ustawi wa chama na nchi kwa ujumla wake. Ni muhimu kukumbuka kuwa siku zote majuto ni mjukuu. Na vita vya panzi huwa ni furaha kwa kunguru. Siku zote vyama vikongwa barani afrika hung'oka madarakani kutokana na magomvi ya wao kwa wao kama ambavyo tumeanza kushuhudia yanayotokea katika Chama cha Mapinduzi CCM.
Hivi ndivyo nianavyo mimi.

KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD

KARIBU KWENYE BLOG YETU YA KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD