Jumatano, 29 Machi 2017

Dkt. JOHANSEIN RUTAIHWA: KIATU CHA UBUNGE WA AFRIKA MASHARIKI KINANITOSHA, NIVALISHENI NIWATUMIKIE



Nafasi ya ubunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni sehemu mojawapo ambayo nchi inapata wawakilishi wake katika Jumuiya hiyo ukiachana  na nafasi ya ajira za moja kwa moja zitolewazo na Jumuiya hii. Ni sehemu nyeti sana kwa nchi katika kupata watetezi kwenye masuala yanayohusu nchi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hawa ni wawakilishi wetu hatupaswi kufany makosa kwenye teuzi zao, tunapaswa  tuchague watu makini wenye uwezo wa kuliwakilisha vyema taifa letu. Hatutakiwi kuruhusu nchi yetu imezwe na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki. Mchango na umuhimu wa Tanzania kwenye nchi za Afrika Mashariki, kati na Afrika kwa ujumla wake lazima ubaki pale pale kama ilivyokuwa enzi za Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere. Tunataka Tanzania iwe kigezo kwenye nyanja zote kisiasa, kiuchumi, kijeshi na kijamii. Maslahi ya Taifa kimataifa yanategemea zaidi uwezo wetu wa kushawishi.
Kutokana na umuhimu huo kwa taifa, tunahitaji wawakilishi wanaojiweza katika kushawishi, wanaojua historia yetu, vipaumbale vyetu lakini vilevile wanaofahamu vyema lugha ya kingereza ambayo ndiyo lugha rasmi ya mawasiliano ndani ya jumuiya hiyo. Kwahiyo tunapotafuta wawakilishi lazima tuangalie ujuzi wao kwenye kuzungumza lugha ya kiingereza na uwezo wao wa kushawishi kupitia ujenzi wa hoja madhubuti zenye uzito na mashiko.

Hatupaswi kukosea kwenye maamuzi. Ukubwa wa nchi yetu lazima uakisi uwezo wetu. Na ushawishi tulionao kwenye nchi za Afrika mashariki na kati toka enzi lazima tuudumishe. Tunataka Tanzania ibaki kuwa kitovu na tegemeo kwa nchi zote zinazotuzunguka. Ili kuyafikia malengo hayo watu wenye mamlaka lazima watutafutie watu wenye uwezo, watu ambao watalitendea haki taifa letu hasa kwenye masuala yote yanayohusu nchi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Tunahitaji busara za wazee lakini hatupaswi kuziweka kando damu changa za vijana wetu wasomi, wachapakazi na wazalendo wakweli kwa nchi na wanaojua wajibu wao na walio tayari kukesha macho usiku kucha kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi yetu.
Miongoni mwa vijana makini waliyotia nia katika kuwania nafasi hiyo nyeti ya ubunge wa bunge la Afrika Mashariki kwa mwaka 2017/18 hadi 2021/22 ni Dkt. Johansein Rutaihwa. Huyu ni kijana kindakindaki wa chama cha Mapinduzi, mpenda mageuzi na ni msomi wa kutegemewa. Mtu wa watu anayependa kufanya utafiti kabla ya kuamua. Mwenyewe amesema…… “ Nimedhamiria kulitumikia taifa langu kupitia elimu yangu, maarifa yangu, na uzoefu wangu katika masuala ya kimataifa. Uamuzi huu nimeuchukua baada ya kujitathmini kwa kina na kujipima kwa muda mrefu na hatimaye kubaini kuwa kiatu cha ubunge wa Afrika mashariki kinanitosha, nivalisheni niwatumikie”
Vilevile Dkt. Johansein aliwaomba watanzania wamuunge mkono katika harakati zake za kuwania ubunge huo wa Afrika Mashariki na alihaidi kutowaangusha ……. “Naamini katika uwezo wangu na katika hili sitowaangusha, endeleeni kuniunga mkono, najua dhamana kubwa niliyonayo kwa Watanzania ziadi ya 52 milioni. Tunahitaji damu changa kuleta mabadiliko ya kweli”. Kaulimbiu yake anayoitumia katika kinyang’anyiro hicho ni kuwa…… “Tusimame pamoja, taifa kwanza”
Katika kutaka kujua Dkt. Johansein Rutaihwa ni mtu wa aina gani, nilijaribu kuongea na watu mbalimbali, wakiwemo watu waliopata kusoma nae katika ngazi mbalimbali za elimu, kufanyakazi nae, majirani na hata wazazi wake. Kwa hakika watu wote nilio ongea nao hawakusita kumwagia sifa kemkem kutokana na tabia yake nzuri kwa jamii anayoishi nayo. Wengi walisema Johansein ni mtu wa msaada sana na mara nyingi huwa habagui kila mtu ni rafiki yake shida yoyote inayompata mtu mwingine yeye huichukulia shida hiyo kama yake. Laiti nafasi ingeruhusu ningeweka shuhuda za watu mbalimbali lakini kwa sababu ya muda nitaweka shuhuda chache tu.
Mtu wa kwanza kabisa kufanya nae, maongezi alikuwa baba yake mzazi, Mzee Rutaihwa yeye kwa upande wake nilimuuliza anamuongeleaje mwanae Johansein akiwa kama Baba aliye mlea toka utotoni hadi anakuwa mkubwa, nilitaka kujua kijana wao ni mtu wa aina gani hasa ukilinganisha na watoto wake wengine. Mzee RutaIhwa yeye aliniambia…... “sikiliza Bwana Aman, mimi nina watoto wawili tu na wote ni wa kiume halafu wamepishana sana kwa tabia yaani huyo mkubwa ana mambo yakwake na Johansein ana yakwake, sasa Johansein moja ni msikivu, yaani lile jambo unaloweza kulisema na kuliona kama la kawaida tu kama mzee, yeye analichukulia kwa uzito wa pekee, ukijakupata habari baadae unakuta anakuambia unajua Baba ulianimbia kitu fulani, sasa mimi wakati mwingine nakuwa nimekwisha kusahau, hivyo yeye ndiye kwanza anakuwa ananikumbusha, pili ambalo naweza kulikumbuka upesi ni kwamba Johansein huwa ni mtu wa kufanya utafiti kabla ya kufanya jambo, yaani huwa hakurupuki, na ndiyo maana huwa hakosei yupo radhi kutafuta ushauri kwa wengine ili kufanikisha jambo lake”…… Mzee Rutaihwa aliongeza kusema,………“Kitu kingine ni kuwa Johansein ni mtu wa kutegemewa, ikitokea imetolewa kazi katika kundi na yeye yupo basi tegemea kupata matokeo mazuri”
Kwa upande wake bwana Ally Amos kijana mmoja wapo aliyesoma na bwana Johansein Rutaihwa kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari ya Umbwe nae alikuwa na haya ya kusema………. “ Nampongeza sana Johansein kwa uamuzi sahihi na dhamira nzuri aliyokuwa nayo katika kuitumikia nchi yake na kuwakilisha taswira nzuri kwa vijana wa Tanzania, namfahamu jinsi alivyo na utu, busara, hekima, kipaji cha uongozi na dhamira nzuri ya kuona kila kijana anatimiza ndoto zake za maendeleo. Mungu amwongoze na amvushe kwenye kila kikwazo mbele ili taifa liweze kunufaika na vipawa vyake”
Naye Dkt. Godfrey Nyamrunda ambaye alipata kusoma na bwana Johansein Rutahiwa katika ngazi ya Chuo kikuu kwa upande wake alikuwa na haya ya kusema……….. “Aaaaah sikia bwana nikuambie, Johansein ni mtu very researchful kwa maana ya mtu anayependa kujifunza vitu kwa undani na ni mtu ambaye ni mwamini mzuri sana wa sera za Chama Cha Mapinduzi naweza kusema ni mjamaa mzuri na mtu anayesimama kukitetea Chama. Jamaa naweza kusema ni mtu wa watu ni mtu anayejua kujichanganya na watu katika masuala mbalimbali ya kijamii. Ni msikivu lakini ni mtu anayependa kusaidia wengine kwa hali na mali pale inapotokea kuna uhitaji huo. Naamini ikitokea nchi ikampa ridhaa ya kuwa mbunge wa bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki basi itakuwa imepata mtu fasaha kabisa wa kuwakilisha maslahi ya nchi katika Jumuiya hiyo”
Sifa za Dkt. Johansein Rutaihwa zimetamalaki kila kona kuanzia alikosoma, maeneo mbalimbali aliyopitia katika utendaji pamoja na nyumbani anakoishi. Taifa linahitaji mwakilishi wa aina ya Dkt. Johansein, mtu anayetanguliza maslahi ya taifa mbele kuliko maslahi yake binafsi, mtu anayetazama shida ya mwenzake kama shida yake.
Unaweza ukajiuliza hivi Dkt. Johansein ni nani hasa, ametokea wapi na ni upi uzoefu wake katika masuala ya kimataifa.
Dkt. Johansein Rutaihwa ni kijana wa kitanzania aliyezaliwa mwaka 1982, Mkoa wa Kagera wilaya ya Bukoba Vijijini, Kata ya Katoma, Kijiji cha Kaishemarwa. Mwaka 2009 alihitimu shahada yake ya uzamili katika Sera na Sheria za biashara za kimataifa kutoka chuo kikuu cha LUND kilichopo nchini SWEDEN. Mwaka 2007 alihitimu shahada yake ya kwanza ya Sanaa ya Uchumi kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam.
Bwana Johansein amepata tuzo mbalimbali za kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kutunikiwa Shahada ya ya heshima ya Uzamivu ya maendeleo ya uchumi yaani “Honory Doctorate on Economic Development “ya Baraza la Kisayansi la taaluma ya Sayansi ya mashariki ya Ulaya. Ukraine, kutokana na kutambua mchango wake wa uandishi katika eneo la biashara, uwekezaji na viwanda. Aidha, alitunukiwa Tuzo ya heshima na Rais wa China kupitia idara ya mahusiano ya kimataifa ya chama tawala cha China “The Communisty Party of China (CPC)” kwa kutambua mchango wake katika masuala ya maendeleo.
Uzoefu wake katika siasa ukoje?
Bwana Johansein Rutaihwa ni mwanachama hai wa chama cha Mapinduzi toka mwaka 2005 hadi leo akiwa na kadi ya jumuia ya vijana ya CCM yaani UVCCM namba 652829 na ile ya uanachama wa chama cha mapinduzi CCM namba Ab1293691. Alishiriki kwa kikamilifu katika uchaguzi wa mwaka 2005 uliomuingiza madarakani Mhe.Jakaya Kikwete,Rais mstaafu wa awamu ya nne.Akiwa na makada wengine walizunguka nchi nzima kuwashawishi wananchi wachague CCM, na aidha ndio waliandaa ripoti iliyokuja kuanzisha Shirikisho la wana CCM vyuo vikuu.
Uzoefu wake Kitaaluma Katika Taasisi na Mashirika Mbalimbali
Bwana Johasein Rutaihwa amefanya kazi katika mashirika na taasisi mbalimbali kuanzia mfuko wa maendeleo wa kujenga tafiti za afrika mashariki (EARCDF) kama Mshiriki katika Utafiti, Wanawake katika Ujasiriamali (WISE) kama “Youth Think Tank”, SIKIKA kama Afisa Programu Msaidizi, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Tanzania kama Mchumi na Katibu binafsi wa Waziri, REPOA kama Afisa Utafiti, Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kama Mtafiti Msaidizi, na kwasasa Dkt. Johansein Rutaihwa anafanya kazi katika shirika la Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) kama Mratibu wa Mradi wa kuwajengea uwezo sekta ya umma na binafsi katika kuandaa, kutekeleza na kutathmini sera za viwanda. Mradi huu unatekelezwa na UNIDO kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki na unahusisha nchi zote tano.
Makala haya yameandikwa na Aman Ng’oma
Simu 0767989713
Dodoma.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD

KARIBU KWENYE BLOG YETU YA KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD