Tulipata fungu la kuboresha barabara za mitaa ya Songea Mjini lakini cha kushangaza hata kuwasimamia makadarasi tuliyowapa kazi wenyewe tulishindwa hadi Mkuu wa mkoa mpya, Mama Mndeme amekuja kuwatimua. Madiwani tuliyowachagua wapo tu wanatazama, hawajui hata wajibu wao. Mkuu wa mkoa mpya asingekuja maana yake uozo huo usingeonekana!
Watu waliyopewa dhamana hawawajibiki ipasavyo. Tunapaswa kuwa kitu kimoja na tuzungumze lugha moja. Tukiondoa maslahi binafsi na tukatanguliza mbele maslahi ya mkoa wetu
kwa kila Mwanaruvuma kwa nafasi aliyonayo, naamini vizazi vyetu vijavyo vitatukumbuka kwa maamuzi mazuri tunayoyafanya sasa.
Ruvuma ni lulu ya nchi. Tena ni lulu kwelikweli. Taifa linaitegemea kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kutokana na kuwa na hali ya hewa nzuri, hali ya hewa inayoruhusu uzalishaji wa mazao mbalimbali, uchapakazi wa wananchi wetu unaosukumwa kutoka ndani ya mioyo yao unaongeza chachu ya ukuaji wa kilimo. Ndiyo maana siku zote wananchi wa Ruvuma huwezi kuwasikia wakilia njaa, bali utakachowasikia wakilia ni kukosa masoko ya uhakika kwaajili ya kuuza mazao yao. Mwana Ruvuma humtumi kazi, kufanyakazi ni jadi yake. Ndiyo maana hata sera ya Rais wetu Dokta John Pombe Magufuli ya hapa kazi tu haimpi tabu mwananchi yoyote wa Mkoa wa Ruvuma kwani wamezoea Kufanya kazi.
Ruvuma imebarikiwa hasa na Mwenyezi Mungu. Tuna utajiri mkubwa wa madini kuanzia Makaa ya Mawe kule Mbinga, madini ya Urani kule Namtumbo nk. Naamini kama Serikali itaamua kwa dhati kabisa kuwekeza kwenye tafiti za madini na rasilimali nyinginezo za ardhini, bila shaka tutashangwazwa na utajiri utakaoibuliwa. Ruvuma ina kila kitu.
Kinachotakiwa kufanywa ni kuhakikisha kuwa watu wa mipango miji wa mkoa wa Ruvuma wanatengeneza mazingira yatakayovutia uwekezaji mkoani kwetu. Kazi kubwa ni kutengeneza mazingira tu, Wawekezaji wako wengi sana, wakiona mazingira yako vizuri watakuja tena kwa kukimbia. Ni sisi tu tunapaswa kujua namna ya kuwatengenezea mazingira rafiki na kuwahakikishia usalama wa mitaji yao watakayoiwekeza.
Maeneo ya uwekezaji ni mengi, kuna kilimo, Supermarkets, MALL za biashara, Mahotel makubwa, Vitega uchumi, Mabustani ya kupumzikia, Maviwanda makubwa ya kuzalisha na kusindika bidhaa mbalimbali, Uwekezaji katika sekta ya Utalii nk
Kufanikisha hili ni muhimu miundombinu ya mjini hasa barabara za mitaa zikatengenezwa vizuri huku pembeni ziking'arishwa kwa taa za barabarani. Kila kitu kinawezekana ni mipango tu.
Kwa sasa nina imani kubwa na mkuu wetu mpya wa mkoa Mama Mndeme, naamini kupitia yeye atatuvusha na tutafika salama tunakoenda ila kitu cha muhimu, madiwani wetu wanapaswa kutambua wajibu waliyonao kwa mustakabali wa maendeleo ya mkoa wetu. Wao ndiyo wasimamizi wakubwa wa miradi yote ya maendeleo ya mkoa. Wao wakilala wajue kila kitu kimelala. Watu wamekalia makundi yasiyokuwa na msingi wowote badala ya kuangalia ni namna gani Ruvuma itaendelea. Pongezi kubwa kwa Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassimu Majliwa Kassimu kwa kuona tofauti za madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Huu ni mfano tu ambao hata halmashauri nyingine za mkoa wa Ruvuma zikimulikwa lazima utakutana na tofauti hizi za maslahi binafsi zikiwa zimetamalaki.
Serikali yetu imejitahidi kuufungua Mkoa wetu wa Ruvuma kwa barabara za lami na kwa sasa tunaletewa mradi mkubwa wa grid ya taifa ya umeme, tunashukuru kupitia mradi huu, vijiji vingi vya mkoa vimeweza kunufaika. Kukamilika kwa mradi wa REA, ni ishara tosha ya mwanzo mpya wa maendeleo endelevu mkoani kwetu.
Tunaishukuru sana Serikali yetu kwa jitahada kubwa inayoifanya ya kuufungua mkoa wetu wa Ruvuma hasa kwenye upande wa Miundombinu. Hali sasa imeimarika sana ukilinganisha na siku za nyuma. Hatahivyo, bado tunaendelea kutoa maombi kwa Setikali yetu dhidi ya barabara kuu ya Njombe hadi Songea Mjini. Tunatamani na yenyewe iweze kutazamwa kwa jicho la kipekee. Barabara imekuwa finyu na imechoka ile mbaya. Barabara toka enzi ya mkoloni hadi leo bado iko vilevile, kwakweli inahitaji kutafutiwa fungu mahsusi ili ijengwe upya na ilete sura mpya. Naamini kama itajengwa upya hata ajali zitapungua sana hasa kwa kuzingatia hatari ya barabara yenyewe ilivyo.
Nawasilisha
Aman Ng'oma
*Mkereketwa wa Maendeleo Ruvuma*
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni