WATANZANIA HATUJIKUBALI, HATUJIELEWI ,HATUNA UZALENDO. NANI ANABISHA?
NA EDO KUMWEMBE
NCHI inaliwa usiku na mchana. Unajua kwanini? Achilia mbali tamaa
binafsi zilizojaa katika mioyo yetu, lakini asilimia kubwa ya Watanzania
hatuitazami nchi yetu katika jicho la uzalendo.
Huyu
anashirikiana na mzungu kuingia mkataba duni wa Madini, yule
anashirikiana na mgeni kuingia porini kuua Tembo na kutoweka na meno
yao. Matokeo yake barabara nzuri za Lami zinajengwa Ulaya, vijijini
kwetu tunaachiwa mashimo.
Kwetu sisi, mtu akipata kazi TRA
tunamwambia ‘Kazi kwako, ushindwe mwenyewe kujenga sasa’. Hii ndio
Tanzania kadri niijuavyo. Mtu hana habari kwamba huyo mtu anayemshawishi
kujenga ndiye mwenye mamlaka ya kusimamia kodi zetu.
Uzalendo ni neno gumu kwa Mtanzania. Hata katika michezo ni hivyo hivyo.
Mwaka 2006, mgeni mmoja alisafiri kilomita 8945 kutoka
Rio de Janiero mpaka Dar es salaam kwa ajili ya kuwafundisha Watanzania jinsi ya kuipenda timu yao ya taifa.
Ni Marcio Maximo. Mbrazil huyu alisafiri kutoka kwao kuja
kutuelekeza jinsi ya kuvaa jezi za Taifa Stars, jinsi ya kuvaa skafu,
jinsi ya kushangilia wachezaji wetu uwanjani. Aibu iliyoje! Mpaka leo
Watanzania wanakiri hili hadharani. Kwanini tulishindwa kulitambua hili
kabla hajafika?
Wakenya wana matatizo yao. Lakini nje ya
matatizo yao, Mkenya akimuona mwenzake, basi anajihisi kama anajitazama
mwenyewe. Ni kama ilivyo kwa Waingereza, Wacongo, Wamarekani, Wanigeria
na wengineo.
Wanamuziki wa DR Congo kazi yao kubwa ni
kusifia watu wao. Nyakati Fulani nilikuwa nasikiliza nyimbo zao na muda
mwingi walipenda kumtaja Dikembe Mutombo. Staa wa zamani wa Kikapu wa
NBA aliyezaliwa Kinshasa.
Umewahi kumsikia Mwanamuziki wa
Tanzania ameimba wimbo na kumtaja Hasheem Thabeet? Katika ubora wake wa
sasa hivi, umewahi kufikiria Diamond Platinum anamtaja Hasheem katika
wimbo wake walau mmoja?
Lakini pia umewahi kufikiria katika
mahojiano yoyote ambayo Hasheem anaweza kufanya na CNN au kituo
chochote cha Televisheni duniani anaweza kusema anavutiwa na nyimbo za
Diamond au Juma Nature ambaye alikuwa akimpenda sana wakati yupo shuleni
Makongo? Hapana.
Sehemu ya ndani ya mioyo yetu haitutumi kujipenda. Inatutuma kuwapenda zaidi wengine. Kama Hasheem Thabeet angekuwa Mkenya,
Watanzania tungemfuatilia kwa umakini zaidi.
Na ndio maana kwa kufuta ujinga huu, nilianza kwenda Lubumbashi
kwanza kueleza jinsi Mbwana Samatta anavyoishi kifahari nchini humo,
kabla ya kwenda Italia kueleza jinsi McDonald Mariga anavyoishi.
Tanzania kwanza, Afrika Mashariki na dunia baadae!
Mara kadhaa katika mahojiano yake na vyombo vya habari, Obi Mikel
huwa anasema anavutiwa na wanamuziki ndugu wa kundi la P Square. Na
wanamuziki hawa wakihojiwa kuhusu wanasoka wanaowapenda huwa wanaanza na
Obi Mikel. Wote ni Wanigeria hawa. Kwao, maisha yanaanzia nyumbani!
Carlos Tevez akifunga bao huwa anaonyesha fulana yake ya ndani
iliyoandikwa jina la Fuerte Apache. Hiki ndio kitongoji alichotoka pale
Buenos Aires, Argentina. Lakini umewahi kufikiria kwamba siku moja
Samatta atavua jezi yake na kutuonyesha fulana iliyoandikwa
Mbagala, eneo alillokulia? Hawezi kufanya hivi. Hajafundishwa uzalendo.
Na wakati mwingine unajiuliza, kwanini umlaumu wakati hata nyumbani
kwake pale Lubumbashi sebuleni hakuna bendera ya Tanzania?
Watu wanaochota pesa Serikalini kwa madai ya kuitangaza Tanzania
wamewahi kuwasiliana naye? Majuzi kulikuwa na picha imeenea katika
mitando mbalimbali ya kijamii ikimuonyesha Robin van Persie na Hasheem
Thabeet wakiwa wamepiga picha jijini London. Ni Van Persie mwenyewe
ndiye aliyekuwa ameituma picha hiyo katika mitandao. Cha ajabu, kuna
baadhi ya Watanzania walianza kuhisi kwamba picha hiyo ilikuwa
imetengenezwa tu kiubunifu na watu wa mitandaoni. Aibu iliyoje!
Kuna ajabu gani mwanasoka nyota wa Ligi Kuu ya England akapiga
picha na mchezaji kikapu wa NBA. Au kwa sababu mcheza kikapu huyo ni
Mtanzania? Kujidharau kulikopitiliza.
Wakati Francis Cheka
alipompiga bondia wa Marekani, Phill Williams Agosti mwaka huu,
mashabiki wakaanza kukejeli kwamba Cheka
alikuwa amempiga
Kinyozi tu kutoka Marekani. Ni kweli kwamba Williams anamiliki Saluni
nchini Marekani. Lakini si hata Cheka anaokota chupa za maji pale
Morogoro? Wote ni mabondia wa kulipwa lakini wana shughuli zao nje ya
ulingo wa ngumi. Hata hivyo kwa sababu Cheka alishinda, tukatafuta
sababu kuwa Williams ni kinyozi. Lakini Cheka angedundwa tungemkejeli tu
kuwa hajui ngumi.
Ndivyo tulivyo Watanzania. Mgeni kwanza, mwenyeji baadae.
Pambano la Flyod Mayweather na Canelo Alvarez wa Mexico lilijaza
marafiki kibao wa Mayweather ambao ni mastaa kama vile Puff Daddy, Lil
Wayne, Denzel Washington na wengineo. Hapo ilikuwa Marekani kwanza. Sisi
hapa Cheka akishinda tunanuna.
Matokeo yake nchi inaliwa
taratibu na sasa ni kama vile tumechelewa. Kila mtu anaishia kujitazama
yeye. Hakuna anayeitazama nchi kama nchi. Uzalendo wetu uko chini sana
wakati kwa wenzetu uzalendo ni sawa na ngozi na mfupa.
Karibu kila kitu kilichokwama hapa nchini, tatizo lake kubwa la msingi
ni uzalendo. Mengine yote yanakuja baadae. Hatuipendi nchi yetu. Hatuna
ufahari nayo. Hatujikubali. Hatujielewi. Hatuna uzalendo. Nani anabisha?
Source: Mwanaspoti
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni