Leo nina furaha kubwa sana kwani baada ya safari ndefu na yenye
changamoto nimerudi nyumbani kuwasalimu wananchi wenzangu! Na hii si
salamu za kawaida bali nawasalimu kwa salaam za demokrasia, uadilifu,
uzalendo na uwajibikaji.
Nawasalimu si kama mbunge bali kama mwana wenu wa Kigoma! Na popote
niendapo najivunia kujitambulisha kama Mtanzania; kama mwenyeji wa mkoa
wa Kigoma na zao la Ujiji.
Tuna mengi ya kujivunia kama taifa lakini Ujiji na watu wake mna nafasi
ya pekee katika historia. Watu wa Ujiji mlipokea harakati za kudai uhuru
wa nchi yetu mapema kabisa mapambano ya uhuru yalipoanza. Watu wa Ujiji
mlikuwa wa kwanza kabisa kupokea mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Na
Jimbo la Kigoma Mjini ilikuwa miongoni mwa majimbo ya mwanzo kabisa
kutoa mbunge wa CHADEMA mwaka 1995. Kabla ya hapo mlitoa madiwani wengi
mwaka 1994.
Wakati Watanzania wengine wakiwa wanajiuliza mara mbili mbili kuhusu
kujiunga na vyama vipya vilivyoanzishwa, watu wa Ujiji, watu wa Kigoma
hamkusita kupokea mabadiliko. Wengi wamepoteza maisha yao, wengine kazi
zao na wengine hata ndoa zao katika kupata mbegu ya mabadiliko katika
nchi yetu. Nawataka msichoke. Wekeni nguvu mpya katika kusimika
mabadiliko kwani bado kazi ya kuimarisha demokrasia katika nchi yetu
haijaisha na inahitaji uvumilivu, kusameheana na kuaminiana.
Na nchi yetu Tanzania ni nchi inayoonyesha uwezo mkubwa katika
kupendana, kuaminiana, kuvumiliana na hata kusameheana. Na haya si
maneno tu ambayo ninayazungumza kama mwanasiasa. Hii ni hali halisi na
maisha niliyoyaishi kwa mifano nilipokuwa ninakua na kusoma katika shule
ya Msingi Kigoma na baadaye Shule ya Sekondari Kigoma.
Malezi yangu yalikuwa yanaongozwa na jamii nzima ya Kigoma. Nimekuwa
nikiwaeleza rafiki zangu niliokutana nao kwenye masomo na kwenye siasa
kwamba nimeanza kuvaa viatu kwa mara ya kwanza nikiwa darasa la tatu.
Viatu hivyo viliitwa 'asante Salim' vilivyokuwa vinatengenezwa na
Kampuni ya Bora Shoes. Vililinunuliwa na mama Coretha Furugunya ambaye
tulikuwa tunakaa mtaa mmoja wa Kisangani Mwanga. Mama Coretha
hakuninunulia viatu kwa sababu alikuwa ana uwezo mkubwa, la hasha!
Alifurahishwa na matokeo yangu ya mitihani ya darasa la pili kwenda la
tatu. Ninaamini kitendo cha mama huyu ni ushahidi wa uungwana, upendo na
hata uwajibikaji ambao tunao sisi watanzania.
Uwajibikaji kwani alichukua jukumu kunilea ingawa hakuwa mzazi wangu,
lakini aliona kuwa kama mwanajamii ana nafasi kubwa katika kuwaendeleza
watoto wote. Jamii hii ya watu wa Kigoma ilinifunza kuwa nikijitahidi na
kukazana kwa bidii kwenye masomo na majukumu, nitafanikiwa. Siwezi
kusahau somo hili katika maisha yangu na ni somo hili ndilo limenifanya
nijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuwatumikia kwa uadilifu na
mafanikio ya hali ya juu sana.
Nikiwa nimejaa matumaini haya kuhusu wananchi wenzangu, leo nataka
niwakumbushe kwa nini kama jamii tulichagua kufuata njia ya demokrasia.
Demokrasia ina maana pale ambapo inatumika kuleta mabadiliko chanya
kwenye maisha ya wananchi. Maisha yanayotakiwa ni yale yanayomwezesha
mwananchi kupata huduma zake stahili kama Elimu, Afya, Maji na
miundombinu. Demokrasia haina maana pale wananchi wanakufa njaa kwa
kukosa ajira na kukuza umasikini. Demokrasia inahusu maendeleo.
Tumejitahidi kwa upande wetu kuondoa mkoa wa Kigoma kutoka mikoa isiyo
na miundombinu kabisa ya maendeleo mpaka kuwa mkoa unaotumika kama mfano
kwa miradi mingi ya Maendeleo ikiwemo Daraja la Malagarasi, Uwanja wa
ndege wa Gombe-Mahale, barabara za lami na upanuzi wa Bandari, ujenzi wa
bandari ndogo mpya na ujenzi wa kituo cha Usafirishaji Mwandiga.
Asije mtu akasema yeye ndio kafanya haya. Haya ni matunda ya nyinyi watu
wa Kigoma kupokea demokrasia na bila woga kuchagua viongozi wenu bila
kujali vyama bali kwa kuangalia uwezo. Haya ni matunda ya viongozi wenu
kupaza sauti yenu kwenye baraza la Taifa, Bunge. Haya ni matunda ya
uvumilivu wenu na uamuzi wenu wa kutaka maendeleo. Juhudi hizi lazima
ziendelezwe kwa nguvu zote ili kuhakikisha kuwa nafasi ya mkoa wa Kigoma
katika uchumi wa Tanzania inaonekana dhahiri na hivyo kuchochea
maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa kituo cha biashara katika nchi za maziwa
makuu.
Lakini tukumbuke pia kuwa Demokrasia ni Uwajibikaji. Katika kipindi cha
utumishi wangu kwenu,kutokana na malezi niliyoyapata kutoka
kwenu,nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa Serikali inawajibika kwa
Wananchi. Nakumbuka wakati napambana kuhusu sheria mbovu ya madini kuna
watu hapa nyumbani walisema 'sasa huyu kawa mbunge wa Taifa' lakini
watu wengi zaidi wakasema tumemtuma Dodoma kusemea Watanzania wote na
sio Kigoma tu.
Tuliweza ndani ya miaka mitano kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye
sera ya Madini na sheria ya madini ambapo baadhi ya mambo ambayo
yalikuwa hayafikiriki sasa yametungiwa sheria ikiwemo Serikali kuwa na
hisa kwenye migodi, Tanzanite kumilikiwa na Watanzania sio chini ya
asilimia 50 na kuzuia kabisa wageni kuchimba vito vya thamani.
Uwajibikaji ulipelekea kumshinikiza Rais kufanya mabadiliko makubwa ya
Baraza la Mawaziri kwa kuwafukuza mawaziri wanane mwaka jana. Hii
ilitokana sio tu na hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu bali pia
ushiriki mkubwa wa wananchi kupitia simu na mitandao ya kijamii ambapo
wabunge walishinikizwa kuweka saini kwenye karatasi za kumtoa Waziri
Mkuu. Toka wakati huo kumekuwa na utaratibu sasa ambapo wabunge hawaoni
taabu kutaka uwajibikaji waziwazi ili kuzuia ubadhirifu wa fedha za
Umma. Ni hivi jana tumeshuhudia mawaziri wanne wamejiuzulu na kufukuzwa
kazi kutokana na kashfa ya operesheni Tokomeza ujangili iliyoibuliwa na
ripoti ya kamati ya bunge. Mabadiliko haya ni hatua muhimu katika
kuimarisha demokrasia yetu.
Pamoja na matunda haya mengi mazuri lakini bado kuna changamoto katika juhudi zetu.
Changamoto kubwa tuliyonayo wananchi ni kukosekana kwa imani katika demokrasia yetu.
Kutoaminiana
Ni dhahiri kuwa kutoaminiana katika nchi yetu kumekuwa kwa kiasi
kikubwa. Taarifa za kitafiti zinaonyesha kuwa katika kila Watanzania
kumi, wanane hawaaminiani. Ni changamoto kubwa sana. Wananchi wameacha
kutuamini wanasiasa na wanasiasa wameacha kuaminiana wenyewe kwa
wenyewe. Hivi sasa uongo umegeuzwa kuwa ukweli na ukweli umekuwa ni
uongo. Hivi sasa ukitaka kuwa mwanasiasa maarufu inabidi ujue kudanganya
na ukitaka kuitwa mwanasiasa msaliti inabidi uwe msema kweli.
Kukosekana kwa uaminifu na kuaminiana imekuwa ni kansa katika siasa
zetu. Itachukua muda mrefu sana kujenga demokrasia imara katika nchi
yetu kama hatutapata jibu la changamoto hii ya kutoaminiana na kugeuza
uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo. Hivi sasa ukweli umekuwa
unatengenezwa badala ya kutafutwa. Ni majanga! Juzi bungeni Mwanasheria
Mkuu wa Serikali alielekeza shutuma kwangu kwamba sikushirikiana na
kamati maalum iliyoundwa na Bunge kufuatilia mabilioni ya uswisi na
kwamba chini ya kiapo nilisema sina majina ya watu wenye akaunti huko
Uswisi. Huu ulikuwa ni uongo.
Ni uongo kwa sababu niliitika wito wa kamati hata nilipokuwa katika
mafunzo ya mgambo huko Tanga na nilikutana nao mara nne. Ni uongo kwa
sababu niliwapa wajumbe wa Kamati Maalaum maelezo na taarifa nyingi sana
kuhusu utoroshwaji wa fedha nje ya nchi na umiliki wa mali nje ya nchi
kinyumecha sheria.
Ni uongo kwa sababu mimi kutotaja majina haya haina maana sina majina,
bali ni kwamba ninaheshimu utaratibu na nimeachia vyombo husika
vikamilishe uchunguzi. Kwani mimi kama mtu binafsi nikianza kuchukua
majukumu ya taasisi ninaweza kutia dosari harakati hizi muhimu na hata
kupelekea mchakato mzima kuvurugika. Sitaingia mtego huu! Lakini hatua
hii ya Mwanasheria Mkuu imenipelekea kujiuliza maswali mengi kwa mfano
uongo kama huu ulifanywa kwa malengo gani? Na ninajikuta hata mimi
ninaingia katika hali ninayoilalamikia ya KUTOAMINIANA.
Lakini mtambue pia kuwa kutoaminiana kunaleta kutovumiliana. Hivi sasa
kuwa na mawazo tofauti katika vyama vya siasa au hata asasi za kijamii
ni uhaini. Lakini bila kuenzi tofauti za mawazo hatuwezi kujenga vyama
imara wala Taifa imara. Demokrasia imara ni zao la tofauti za mawazo na
uhuru wa mawazo. Kama hatuwezi kujenga vyama vinavyorutubisha uhuru wa
mawazo na tofauti za mawazo, tutajenga Taifa lenye watu wenye kuogopa na
waliojaa woga. Wanachama wanapoogopa uongozi ni udikteta, lakini uongozi unapoogopa wanachama ni demokrasia.
Bila demokrasia ya uwazi na kuvumiliana tutakuwa Taifa la kidikteta.
Lazima vyama vya siasa, viongozwe kwa namna ile ile ambayo Taifa
litaongozwa.
Demokrasia bila kuaminiana, demokrasia bila kuvumiliana sio demokrasia ya kweli
Juzi nilipoingia Bungeni kwa mara ya kwanza baada ya matukio kadhaa
yanayoendelea ndani ya chama chetu nilikaa pamoja na mbunge Tundu Lissu.
Wabunge wengine walidhani tutarushiana ngumi na badala yake ikawa ni
vicheko na mazungumzo. Hii ni kwa sababu sina chuki na mtu yeyote yule.
Mmenifunza kutojenga chuki na watu na badala yake kuchukua kila tukio
kama changamoto ya maisha. Siasa ni kupambanisha mawazo tofauti na
hatimaye kutafuta suluhu ya pamoja. Na siasa ina misingi yake ambayo
sisi wanasiasa huwa tunasahau kwa maksudi. Msingi wa siasa ni kuwa
inapaswa kuleta unafuu wa maisha ya wananchi na sio malumbano tu ya
kurushiana maneno na kuzushiana ili kujijengea umaarufu wa kisiasa.
Siasa si kuwekeana chuki na kuonyeshana ubabe.
Na hapo ni muhimu muelewa wanaKigoma mnapoambiwa kuwa eti ninapofuatilia mabilioni ya Uswisi ninatafuta umaarufu, ni uongo! Mnaposikia eti kukataa kwangu kuchukua posho ni unafiki na kujitafutia umaarufu, ni uongo! Kinachonisukuma kufanya vyote hivi ni ninyi. Ninasukuwa
kila ninapowaona watoto bado wanatembea bila viatu; kila ninapoona
akina mama wanapoteza maisha yao katika uzazi;kila ninapoona vijana
ambao hawana uhakika wa kupata hata mlo moja kwa siku kwa kukosa kazi;
ninapoona wazee wa Kigoma kukosa hata shilingi mia moja kununua chai
asubuhi. Ninawaona si wanaKigoma bali mamilioni ya watanzania wakiishi
katika hali hii. Alafu nalinganisha na taarifa tunazozipata kuhusu
ufujaji na utoroshwaji wa pesa zetu.
Hebu sasa linganisheni na ukweli kuwa ripoti ya kimataifa iliyotolewa
hivi karibuni imeonyesha kuwa mwaka 2010 pekee, jumla ya dola za
kimarekani milioni 1315 (bilioni 1.3), yaani shilingi trilioni
2,113,930,000,000 (sh trilioni 2.1) zilitoroshwa kutoka nchini Tanzania.
Mwaka 2011 kiasi cha dola za kimarekani milioni 817 yani shilingi za
kitanzania zipatazo trilioni 1,315,370,000,000 (trilioni 1.3)
zilitoroshwa. Ripoti hiyo inaeleza kuwa jumla ya fedha za Watanzania
zilizotoroshwa nje ya nchi katika miaka kumi iliyopita zilifikia dola za
kimarekani milioni 4526 (bilioni 4.5) sawa na shilingi za kitanzania
trilioni 7,286,860,000,000 (trilioni 7.3).
Nimewatajia hapa namba chungu nzima na matrilioni na mabilioni
hayaleti maana. Lakini hii ina maana kwamba kiasi cha pesa
zilizotoroshwa katika miaka 10 pesa - robo yake tuingeweza kujenga
barabara ya lami ya kiwango cha juu kabisa kutoka Kigoma mpaka
Dar-es-salaam!
Pesa hizi zingeweza kuajiri na kuwalipa vizuri walimu, madaktari na
wafanyakazi wengine ili kuhakikisha tunapata huduma bora na kutengeneza
ajira bora kwa vijana wetu. Pesa hizi zingeweza kununua madawa muhimu na
kuokoa maisha ya maelfu ya akina mama tunaowapoteza kila mwaka wakati
wa uzazi. Pesa hizi zingeweza kuwanunulia watanzania wote si watoto tu
angalau pea 10 ya viatu. Sasa nikitafakari haya siwezi kuchapa usingizi
mnono na kufumbia macho utoroshwaji wa fedha au matumizi mabaya ya fedha
za umma kwa njia ya sisi wabunge kujilipia posho! Hapana! Nafsi yangu
hainiruhusu kukaa kimya kwa kuogopa kuitwa mbinafsi au msaliti!
Lakini naomba niwasihi kuwa katika nyakati kama hizi za changamoto za
kisiasa jambo la msingi kuliko yote ni kutulia maana hakuna linalotokea
bila sababu. Licha ya kwamba kuna watu wengi wanapaza sauti zao katika
mambo haya lakini pia kuna wengi zaidi ambao wapo kimya lakini wana
mawazo yao, ndani na nje ya chama chetu;ndani na nje ya Serikali na
ndani nanje ya nchi yetu. Ndio maana lazima kuibadili nchi yetu ili
kuweza kuhakikisha kila raia anakuwa na fursa ya kutoa mawazo na fikra
zake zinakuwa huru.
Maisha ni mabadiliko; mabadiliko hayana ukomo; mabadiliko hayazuiliki
kwa sababu bila mabadiliko hakuna ukuaji, bila mabadiliko hakuna
maendeleo. Mabadiliko ni kiu kikubwa cha Tanzania kwa sababu mabadiliko
huleta matumaini. Na kiu hii ni kubwa zaidi kwetu sisi vijana wa kizazi
hiki kipya. Siasa za kizazi kipya cha viongozi ni siasa za majawabu ya
kero za wananchi. Siasa za mabadiliko ni siasa za kujenga na kuimarisha;
ni siasa za kuaminiana na kuheshimiana hata pale mnapopingana kimawazo.
Ninataka tujenge siasa mpya Tanzania;siasa za mabadiliko; siasa
zinazojenga matumaini ya kweli;siasa zinazowajali na kuwajengea uwezo
wananchi wa Tanzania.
Mungu ibariki Tanzania.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni