Wadau, waandishi wengi wa habari wananipigia nithibitishe ikiwa CUF
iliandaa makundi ya wanachama wakamshabikie ZZK mahakamani leo hii.
Taarifa ya namna hii pia imeenea mitandaoni.
Pia viongozi
kadhaa wa CHADEMA wamenipigia kunijulisha kuwa Intelijensia yao
imegundua kuwa vijana wa CUF wamepenyezwa na kwamba wamevushwa T-SHIRT
za M4C na mapanga.
Napenda
kuwajulisha wadau wote kuwa CUF haijapanga wala kutuma makundi ya vijana
kwenda kumshabikia ZZK. Ikiwa pana wanachama wa CUF wameonekana
mahakamani itakuwa wamekwenda kwa Utashi na Matakwa yao.
Sisi
chama Taifa hatujawahi kukutana, kupanga wala kutuma vijana wa CUF
wakasimamie upande wowote katika mgogoro huu. Wakati wa fukuto la HAMAD
RASHID na CUF watu wengi tu raia walifika mahakamani, sie hatukuwa
kuhoji na kutafuta vyama vyao, tuliamini ni watanzania tu.
Ni
ushauri wangu kuwa, panapokuwa na kesi inayovuta hisia za watu
haitajalisha watu hao wanatoka makundi gani, mwenye kutaka kwenda
atakwenda tu.
Ni vigumu kwa chama chetu kukataza wanachama wake
wasihudhurie kesi ya Babu Seya, ya Sheikh Ponda, ya Zitto Kabwe, ya
Samaki wa magufuli n.k., Unapokuwa na chama chenye mamia elfu ya wafuasi
si rahisi kujua mfuasi yupi yuko wapi kwa wakati gani anafanya nini na
ametumwa na nani.
Lakini kwa ajili ya kujenga mshikamano wa
vyama vyetu, tunachunguza taarifa hizo ili kubaini kama ni kweli
palikuwa na wanachama wetu mahakamani na tukiwabaini tutawahoji na kujua
nani aliyewatuma na tutaona hatua za kuchukua.
Ikumbukwe kuwa
mwenyekiti wa chama chetu taifa Prof. Lipumba wakati akisoma maazimio ya
kikao Cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa mwezi Desemba mwaka jana
alieleza kuwa Baraza Kuu la CUF linawaomba CHADEMA wamalize mgogoro wao
haraka ili tuwekeze nguvu za upinzani katika kuunganisha umma kutafuta
katiba ya watanzania katika bunge la katiba, Msimamo wa CUF ni kutokuwa
na upande katika mgogoro huu.
Tunatoa wito kwa viongozi wa
CHADEMA kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama iwapo wataona au
kuhisi kuna mwananchi au mfuasi wa chama chetu amejiingiza katika
mgogoro wao na kwamba amehatarisha amani ili sheria ichukue mkondo wake.
CUF itaendelea kuiheshimu CHADEMA kama taasisi inayojitegemea.
Hatukuwahi kuingilia, kushabikia wala kupinga masuala na maamuzi ya
ndani ya CHADEMA, tukiona pana jambo linatugusa mara zote huwa tunatoa
ushauri wetu tu na sio kuingilia masuala ya ndani ya vyama vingine.
Julius Mtatiro,
Naibu Katibu Mkuu,
Chama Cha Wananchi CUF,
Tanzania Bara.
06 Jan 2014.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni