Kimsingi mambo tunayotofautiana na Mhe. MBOWE
ni haya yafuatayo:-
MATUMIZI YA RUZUKU
CHADEMA hupata ruzuku ya Tshs. 66,000,000 kwa mwezi (Milioni sitini na
sita). Mimi nasema si haba hasa tukizingatia chama kilikotoka. Naamini
kuwa kiasi hiki cha fedha kikisimamiwa vizuri kinaweza kukirahisishia
chama kujieneza katika ngazi zote toka Tawi, Wilaya, Mkoa na Taifa.
Si kweli kwamba matatizo yote yatamalizwa na fedha hizi lakini basi hata
ofisi za chama zinaweza kuwa hai nchi nzima kitu ambacho kwa sasa
hakipo. Mahesabu yanaonesha kuwa mtaji wa laki moja (Tshs.100,000/=) kwa
wilaya moja nchini inatosha, hivyo kwa Wilaya 126 kwa mwezi jumla yake
ni Tshs. milioni 12 (Tshs. 12,600,000/= ) zinahitajika ( Wilaya 126 x
100,000 kila wilaya = 12,000,000/=)Hata tukisema tupeleke kiasi hicho
kwa kila jimbo la uchaguzi jumla yake ni Tshs. Milioni 23 (Tshs.
23,000,000/=) kwa maana ya majimbo 213 x 100,000 = 23,000,000/=.
Mhe. MBOWE anasema hizo ni pesa nyingi sana kwa uimarishaji wa chama.
Mimi nasema hapana, kiwango hiki kwa kila Wilaya au Jimbo la uchaguzi ni
muafaka kwani haba na haba hujaza kibaba.Chini ya uongozi wa Mhe. MBOWE
na wafuasi wake hawastaajabu kuwa kati ya Tshs. 374,144,000.40
zilizopatikana kama ruzuku katika ya Januari 1 na Juni, 30, 2008, Tshs.
350,000,000/= zilitumika Makao Makuu ya CHADEMA na Tshs. 25,000,000/= tu
ndizo zilikwenda Wilayani kuimarisha chama.Mimi naona mgao huu
unayatukuza Makao Makuu ya
CHADEMA isivyostahili wakati huo huo ukidhalilisha chama nchi nzima.
MADENI YA UCHAGUZI
Kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Mhe. MBOWE alitufahamisha
wanachama kuwa alikuwa anakidai chama US $ 181,949.00 sawa na Tshs.
218,338,546. Mpaka sasa chama kimekwisha mlipa Tshs. 175,000,000/=Baada
ya kupata wadhifa wa Makamu Mwenyekiti, na kwa kuzingatia takwimu
zionekanazo hapo juu katika kulinganisha matumizi ya fedha Wilayani na
Makao Makuu niliamua kumshauri MBOWE asitishe kujilipa deni kutokana na
fedha za ruzuku kwani siamini kuwa kulipa madeni yaliyopita kunaendana
na utaratibu wa usimamizi wa fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa toka
serikalini.
Mhe. MBOWE alichachamaa na ndipo nilipomshauri kuwa kama ni hivyo basi
atuthibishie pesa hizo anazodai alikikopesha chama ziliingia kwenye
akaunti gani ya CHADEMA, kupitia hundi ipi, na lini? Nilimuomba pia
kutaja ni kikao gani cha chama kiliidhinisha matumizi ya fedha hizo
kwani kama hakuna ushahidi wa maidhinisho, ni dhahiri kuwa matumizi hayo
hayakudhibitiwa na chama na kwa mantiki hiyo kuyafanya kuwa matumizi
binafsi ya Mhe. MBOWE.Vilevile, nilimueleza kuwa matumizi ya fedha hizo
alizodai alikikopesha chama yalikuwa yakinuka harufu ya UFISADI.
Stakabadhi zote kuhusiana na matumizi hayo zilionesha kuwa gharama za
aidha ununuzi na / au ukodishaji wa vifaa hivyo, hazikutofautiana na
viwango wanavyolipishwa watalii kwa huduma kama hizo, kwa maana ya
gharama ya juu sana.Na kwa kuwa hata baada ya kuwa Mhe. MBOWE amekwisha
lipwa zaidi ya nusu ya deni alilodai kuikopehsa CHADEMA, vifaa vyote
yakiwemo magari, vipaza sauti na kadhalika vimebakia kuwa mali yake
binafsi, basi bila kumficha nilimueleza kuwa huko ni kukinyonya chama
kwa kukigeuza kitega uchumi cha watu binafsi.Kuhusu suala la kulipa
madeni kupitia ruzuku ya serikali, nilimuomba Mhe. MBOWE afuatilie kwa
Msajili wa Vyama vya siasa ili tupate ufafanuzi kama kweli fedha za
ruzuku ya serikali kwa vyama vya siasa, inaweza kutumika kulipia madeni
ya viongozi wa vyama hivyo yatokanayo na uchaguzi ili CHADEMA
isiathirike kisheria.
Niseme kweli hapa kwamba, kwa vile wanaCHADEMA wengi walinichagua kuwa
Makamu Mwenyekiti, na hata mimi mwenyewe tulikuwa wagombea wa nafasi za
ubunge, udiwani n.k katika uchaguzi wa mwaka 2005 ningefarijika sana
iwapo na sisi tungerejeshewa angalau chochote cha kufidia gharama zetu,
kwa maana kwamba kama chama kimeamua kurudisha gharama hizo kiwalipe
wote badala ya kulipa madeni kwa wateule wachache.
UTEUZI WA WABUNGE WA VITI MAALUM
Naamini ukweli wa suala hili hauna mjadala. Kwamba Mhe. MBOWE na wafuasi
wake walighushi orodha ya majina ya viti Maalum badala ya kupeleka
yaliyopendekezwa na Kamati Kuu sio siri.
Naamini hata Mhe. MBOWE anakubaliana nami kuwa suala hili si moja ya
siri anazodai nimevujisha! Yamesemwa mengi juu ya mtafaruku uliojitokeza
kuhusu viti maalum hadi baadhi ya waasisi wa chama wakataka kujitoa na
hivyo kumlazimisha Mwenyekiti Taifa ( FREEMN MBOWE) na Katibu Mkuu (DR
WILBROAD SLAA) kukiomba radhi kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kwa
kukiuka katiba, kanuni na maadili ya chama katika suala hili la kugushi
viti maalum.
Ni ukweli ulio wazi kuwa kitendo hicho cha upendeleo bado kina iumiza
taswira ya CHADEMA. Chama kinaonekana kuendekeza ujanja ujanja kiasi
kwamba watu na binti zao, wakwe zao, shemeji zao, waume wenzao, wachumba
wa shemeji zao, wake wenza na kwa kiwango kikubwa watu wa kabila moja
ndiyo wamekuwa sura ya CHADEMA bungeni.Katika hili nilichoweza kumueleza
Mhe. MBOWE ni kuwa chaguzi mbalimbali tangu za Mitaa, Ubunge na Urais
zinakaribia ni vizuri tufanye bidii kusambaza nguvu zetu nchi nzima tuwe
na mtaji wa kura maeneo mengi ili kashfa kama hii isijirudie. Hii ni
kwa msingi kuwa chama kikijitanua kutakuwa hakuna sababu ya kuwaona watu
wa eneo fulani tu kuwa ndiyo mhimili wa CHADEMA na hivyo zikitokea
fursa itakuwa rahisi chama kuwakilishwa na mtandao wake mpana badala ya
koo au kabila fulani.Sasa kwa kuwa kuimarisha chama kitaifa maana yake
ni matumizi ya fedha, nalo hili likawa nongwa ingawa kwa mtazamo wa
Makao Makuu kulipa madeni kwa wateule wachache si nongwa.
Cha ajabu ni kwamba Mhe. MBOWE hakukana kuwa hili la viti maalum na hata
upangaji wa ajira kwa ukabila una leta athari mbaya kwa mustakabali wa
CHADEMA
Katika maongezi yangu nae nilikuwa wazi nilipotahadharisha kuwa:
1. Watanzania wakiendelea kuona kwamba CHADEMA inaendeshwa kwa misingi
ya kikabila hawatajiunga na chama chetu na tutakosa wafuasi.
2. Watanzania wakiona kuwa sisi tumeweka mbele ukabila kuliko utaifa
hawatatupa madaraka na kutawala kwa kuhofia yale yanayotokea nchi jirani
kama Rwanda, Burundi, Kenya na kadhalika ambako nafasi za raia wote
zimehodhiwa na kabila moja na hatma yake watu wamechinjana kama kuku kwa
kupinga hilo.
Pia nilimwambia kwamba, kwa jinsi sura ya uteuzi wa Wakurugenzi na
watendaji wengine wa Makao Makuu inavyoonekana, sasa tayari chama chetu
kimebatizwa jina la CHAMA CHA WACHAGA, na hii si kuwatendea haki raia
wengine na makabila yao ambao wataonekana kama punguani kujihusisha na
chama na ukabila.Yote haya ninayosema kuhusu ukabila, upendeleo na
kadhalika sio dhana tu. Kufuatia malalamiko mengi yaliyokuwa yakisikika
nchi nzima kuhusu masuala haya, Kamati Kuu ya CHADEMA ilikwisha unda
Tume kutafuta ukweli wa mambo hayo. Tume hiyo ya watu watano iliongozwa
na Mhe. Merky Lugendo Mziray ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA
nayo imekwisha toa taarifa yake kwamba Makao Makuu ya CHADEMA
yanatawaliwa na ubaguzi wa kikabila, kidini na kielimu.