Jumatano, 22 Februari 2017

KUWA NA MABANDA BORA YA KUKU NI MTAJI

Unapofikiria kufanya mradi wa ufugaji wa kuku, hitajio la kwanza na la muhimu ni kuwa na mabanda bora ya kufugai kuku wako. Kwa bahati mbaya sana ujenzi wake umekuwa ghali na hivyo kuwakatisha tamaa watu wengi wanaohitaji kuanza mradi huo.
Katika hali ya kawaida vijana wengi wanaomaliza vyuo vikuu wanakuwa hawana uwezo wa kumudu kujenga mabanda hayo matokeo yake wanashindwa kufanya mradi wa ufugaji wa kuku. Laita kama kungelikuwa na watu binafsi au mashirika ya uma au serikali ikaamua kwa dhati kabisa kuwekeza katika ujenzi wa mabanda bora ya kuku halafu yakakodishwa kwa wahitaji, naamini watu wengi hususani wahitimu wa vyuo wangeweza kuyakodi mabanda hayo na kuyatumia katika biashara hii ya ufugaji wa kuku.
Mabanda ya kuku yanatakiwa yajengwe kwa kuzingatia ubora lakini vilevile na mahali husika yanapotaka kujengwa mabanda hayo ili kujua aina ya mabanda yanayofaa kujengwa kulingana hali ya hewa ya mahali hapo. Maeneo ya joto kwa mfano mikoa yote ya Pwani na Mwambao wa Bahari na Morogoro ni muhimu mabanda yake yakajengwa kwa kuweka madirisha mapana yenye kuruhusu hewa ya kutosha kuingia ndani ya mabanda hayo. Na kwa maeneo ya baridi kwa mfano mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa, Moshi na Arusha madirisha yake yanatakiwa yapandishwe juu sana ili kuruhusu hewa kuingia vyema lakini wakati huo huo kuku waweze kukingwa na hali ya baridi. Lakini kwa maeneo yenye joto kali na upepo wakati wa mchana na baridi wakati wa usiku kwa mfano kwa maeneo ya mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora mabanda yake yanatakiwa yainuliwe kozi sita kutoka msingi kisha juu yawekwe wavu kuzunguka banda lakini wakati huohuo banda hilo lijengwa kwa kukinga upepo na upande ule wa upana kwa kuta zake zote mbili zinapaswa ziinuliwe tofari hadi juu kabisa ili kukinga upepo lakini vilevile paa lake lipande juu sana ili kupooza hali ya joto linalotokana na jua kali wakati wa mchana.
Banda la kuku linatakiwa liwe na hewa ya kutosha ili liruhusu kuku kupata hewa safi. Mara nyingi kinyesi cha kuku kinatoa harufu kali ya amonia inayotengeneza hewa ya kuchomachoma na hivyo kuleta adha kwa kuku wenyewe na Binaadamu halikadhalika.
Kimsingi Muundo wa banda bora lazima liwe na karido kama inavyooneka katika ramani ya banda hapo chini. Korido hiyo inasaidia kufanya wageni wanapoingia bandani wasiingie moja kwa moja walipo kuku na kuwaletea magonjwa. Lakini, hata hivyo, ndani ya korido, pale mlangoni, unapoingia kuna kijidimbwi cha maji ambacho kinachanganywa na dawa ya kuua wadudu na kila mtu anayeingia ndani humo anapaswa kwanza kukanyaga maji hayo ili kuua wadudu wasababishwa magonjwa kutokana na kutembea huku na kule au daktari wa mifugo anapokuja kwako huku akiwa alitangulia kupita kwenye mabanda mengine ya wafugaji na ikatokea mabanda hayo labda yalikuwa na uambukizo wa magonjwa, itasaidia magonjwa hayo yasiingie kwenye banda lako kwa kuwa atakapokanyaga maji yale ya dawa pale mlangoni wadudu wote watakufa na hivyo kuku wako wakabaki katika mazingira salama kabisa. Wafugaji wengi huweka maji ya dawa ya kuulia wadudu nje ya banda mlangoni matokeo yake huwakiwa na jua na hatimae kupunguza nguvu yake na wakati mwingine kukauka kwa haraka. Maji yaliyochanganywa na dawa ya kuulia wadudu kama yakikaa kivulini yatapaswa kubadirishwa kwa wiki mara moja. Na dawa inayotumika kwa ajili ya kuchanganyia kwenye maji ya kukanyaga mlangoni ni V- RID Disinfectant na au dawa nyingine yoyote inayofanana na hiyo itakayoshauriwa na dakatari wako.
Na kama utahitaji michoro ya mabanda mabalimbali ya kuku tafadhali wasiliana nasi kwa gharama nafuu kabisa. Kinasoru East Africa Tanzania Ltd imedhamiria kukupa elimu itakayokufanya uendeshe mradi wako wa ufugaji kwa kwa kujiamini kabisa kutoka na maarifa tunayokupatia.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD

KARIBU KWENYE BLOG YETU YA KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD