Jumatano, 22 Februari 2017

MAFANIKIO YANATAKA UTHUBUTU

Kijana huu ni wakati wako. Jaribu kufanya kila jambo linalowezekana katika kutafuta mafanikio. Usitumie njia za panya, tafuta njia halali njia itakayokufikisha kule unakotaka kufika . Katika kutembea au kupita katika njia hiyo, utakutana na vikwazo vingi, usirudi nyuma songa mbele. Kuwa kama mwanajeshi anapokuwa mstari wa mbele vitani, hakuna kurudi nyuma.
Maamuzi yako ni muhimu ukayasimamia mwenyewe. Si kila mtu anapenda ufanikiwe. Yakupasa kuchagua watu au rafiki wazuri wa kukushauri juu ya mipango yako. Lakini pia unaposhauriwa nawe uwe na akili yako binafsi, akili huru iliyotulia inayoweza kuchuja katika yale unayoshauriwa. Ushauri mzuri chukua na ule usiyofaa ukache mara moja.
Elimu ni nyezo ya kukurahisishia kufika kule unakotaka kufika kwa kukuwezesha kuona fursa mbalimbali. Elimu si lazima iwe ile ya darasani, hata ile ya nje ya darasa inafaa ilimrdi tu ikupe mwanga na uweze wa kuona fursa na kujua namna ya kuziendea. Fedha ni kikwazo kwa watu wengi. Ili utimize malengo yako unahitaji kwanza rasilimali fedha. Namna gani utaweza kupata fedha. Benki hazikopeshi watu wasiyokuwa na dhamana. Hakuna taasisi iliyo wazi kwa ajili ya kusaidia wajasiriamali wachanga.
Nini utafanya. Ni muhimu kidogo ulichonacho uweze kuanza nacho hicho hicho hata kama kwa mradi mdogo. Usikidharau. Wahenga walisema ndondondo si chololo. Jifunze kujiwekea akiba kidogokidogo. Usichague kazi. Ulipo tengeneza vikoba kwa kuwashirikisha vijana wenzako wenye kiu ya kufanikiwa. Mara kwa mara jiwekeeni akiba na kisha mkopeshane wenyewe kwa wenyewe. Uaminifu ni kitu cha msingi sana katika kuyafikia malengo yako.
Kama unaujuzi wowote hakikisha unautumia vizuri, unaweza kuwa mkombozi wako. Tufuta kipawa chako. Kitu gani unakiweza kukifanya kwa ufasaha. Jibidiishe kwenye hicho mwishowe utachomoka.
Futa josho lote linalokutiririka usoni kwako, vumilia jua kali linalokupiga mchana kutwa na mwombe sana Manani muumba wa wote akuongoze vyema katika chaguo lako. Mwishowe ili methali isemayo mchumia juani hulia kivulini itatimia kwako. Na hizi siyo ndoto. Kitu cha msingi usikubali kushindwa. Hapa unapaswa kutambua kuwa hata mtoto ili aweze kusimama ni lazima awe amedondoka sana katika harakati zake za kujifunza kusimama na wakati mwingine, katika harakati hizo, atapata michubuko na kuumia lakini haachi kujifunza kusimama.
Hasara katika mradi au biashara haikwepeki. Kuna watakao kudhulumu katika michakato yako mbalimbali ya kujaribu kuusimamisha mradi wako au biashara yako. Haimaanishi kuwa usifanye mradi huo kwa kuogopa kupata hasara. Hasara ni katika changamoto za kujaribu. Ni sehemu ya kujifunza ulipokosea ili badae usirudie makosa yaleyale. Ndiyo maana ukikaa na yeyote aliyefanikiwa akakupitisha katika mapito yake hakika utatoa machozi.
Mafanikio yanataka uthubutu. Lazima kwanza ujitoe akili na ufanye unachokiamini kuwa kitakuvusha. Ziba masikio usisikilize kelele za watu. Endelea kutumbikiza pesa katika mradi wako au biashara yako bila kujali mara ngapi umefeli au utafeli muhimu ni imani uliyonayo katika huo mradi na jitahidi kufuatilia taarifa za mradi wako mara kwa mara ili upate njia bora zaidi za kuuendea mradi huo ili uweze kuwa na tija.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD

KARIBU KWENYE BLOG YETU YA KINASORU EAST AFRICA TANZANIA LTD